Muswada wa uhamiaji Ujerumani washindwa kupita bungeni
1 Februari 2025Vita vikali vya maneno katika Bundestag, maandamano makubwa mitaani, tuhuma za usaliti na miiko kuvunjwa: imekuwa siku zisizo za kawaida katika siasa za Ujerumani.
Ijumaa, bunge liliukataa kwa wingi mdogo muswada wa kuimarisha sheria za hifadhi ulioungwa mkono na muungano wa vyama vya kihafidhina vya Kikristo vya CDU/CSU, chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD, chama cha waliberali mamboleo cha Free Democrats, FDP, na Muungano wa kipopulisti wa Sahra Wagenknecht, BSW.
Mgombea Ukansela wa CDU Friedrich Merz alifanikiwa kupitisha pendekezo lisilo na nguvu kisheria kuhusu sera za hifadhi Jumatano, akitegemea kwa mara ya kwanza msaada kutoka kwa AfD. Merz alisisitiza kuwa maamuzi kuhusu uhamiaji yanahitajika sasa, bila kujali ni nani anayesaidia kuyafanikisha.
Pendekezo hili lenye utata linataka kuwepo na udhibiti wa kudumu kwenye mipaka ya Ujerumani na nchi zote jirani na kurudishwa watu, hata kama wameomba hifadhi – jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa sheria.
Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni wa Deutschlandtrend uliofanywa na shirika la utangazaji la umma ARD, idadi kubwa ya wananchi wa Ujerumani wanapendelea kuimarishwa kwa sera za uhamiaji. Hata hivyo, idadi kubwa sawa inapinga vyama vya kisiasa kuingia katika makubaliano ya muungano na AfD.
Soma pia:
Zaidi ya majuma matatu kabla ya uchaguzi mkuu wa mapema wa shirikisho tarehe 23 Februari, CDU ina uungwaji mkono wa karibu asilimia 30 na Merz ana nafasi nzuri ya kuwa kansela ajae wa Ujerumani. AfD iko katika nafasi ya pili, ikiwa na karibu asilimia 20. Ijumaa, Merz alikariri msimamo wake wa kutoshirikiana na AfD.
Kansela Olaf Scholz kwa sasa anaiongoza nchi kama sehemu ya serikali ya wachache na chama cha watetezi wa mazingira - die Grüne. Akizungumza na gazeti la Die Zeit Ijumaa, alionya kuwa Ujerumani iko karibu kufuata njia ya Austria, ambapo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Freedom Party (FPÖ) kilishinda uchaguzi msimu wa mapukutiko na sasa kiko katika mchakato wa kuongoza serikali pamoja na Chama cha Watu cha kihafidhina.
Scholz aliliambia gazeti hilo la kila juma kwamba vyama vya kisiasa vya mrengo wa wastani nchini Austria viliahidi mwanzoni kutounda muungano na FPÖ, "...na mwishowe kunaweza kuwa na muungano nao na hata kansela kutoka FPÖ."
Merkel: 'Ni makosa' kutegemea msaada wa AfD
Akizungumza katika mkutano wa kundi lake la wabunge kwenye Bundestag Ijumaa asubuhi, Merz alisema ilikuwa "utunzi" kwamba alikuwa akilenga kufanya kazi na AfD. Hata hivyo, Kansela wa zamani Angela Merkel amechukuwa matazamo tofauti.
Siku ya Alhamisi, alichapisha taarifa akisema kuwa Merz alimhakikishia hivi karibuni kwamba angetafuta tu wingi na vyama vya kidemokrasia vya mrengo wa wastani.
"Ninaamini ni makosa kutojisikia tena kufungwa na pendekezo hili na hivyo, kwa mara ya kwanza, kuruhusu wingi wa kura zinazojumlisha za AfD kwenye Bunge la Ujerumani," alisema, akimaanisha kura ya Jumatano.
Merz, kwa upande wake, alisema katika Bundestag siku ya Ijumaa kwamba nchi hiyo ilifuata sera ya uhamiaji isiyo sahihi katika miaka ya hivi karibuni.
"Na chama changu pia kinabeba jukumu kubwa kwa hili," alisema, bila kumtaja Merkel kwa jina. "Kama tungekuwa tumeifanya vyema wakati huo, AfD isingeingia Bundestag mwaka 2017. Na isingerudi tena katika Bundestag mwaka 2021 pia."
Merz na Merkel wana uhusiano mgumu sana. Mwaka 2002, Merkel alichukua nafasi ya Merz kama kiongozi wa kundi la CDU/CSU katika Bundestag, kisha akawa kansela mwaka 2005 na kumlazimisha Merz mwenye msimamo mkali kuwa nyuma.
Merkel alikiongoza chama hicho na kukiweka katika mrengo wa kati, kwa kukumbatia misimamo kadhaa ya kisiasa ya chama cha mrengo wa wastani wa kushoto cha Social Democratic, SPD.
Akiwa amechoshwa na mwelekeo huo, Merz alijitoa na kujielekeza kwenye sekta binafsi, kisha akarudi tena kuwa kiongozi wa kundi la bunge na kisha kuwa mwenyekiti wa chama baada ya kustaafu kwa Merkel kutoka siasa mwaka 2021.