Muswada wa kudhibiti uhamiaji Ujerumani washindwa bungeni
1 Februari 2025Wabunge wa Ujerumani hapo jana wameukataa muswada wenye utata wa kuimarisha udhibiti wa uhamiaji, na kuzuia ushindi mwingine kwa chama cha siasa kali cha Alternative for Germany, AfD, wiki chache kabla ya uchaguzi wa kitaifa.
Muswada huo uliwasilishwa muungano wa upinzani wa vyama vya CDU/CSU katika bunge la wawakilishi, Bundestag, siku mbili baada ya pendekezo la lisilo na nguvu ya kisheria lililopitishwa kwa msaada wa AfD.
Soma pia: Angela Merkel akikosoa chama chake kwa kushirikiana na AfD kupitisha hoja bungeni
Licha ya kuibua hasira nchini Ujerumani, kiongozi wa CDU/CSU Friedrich Merz alilazimisha kupigia kura muswada wa kukaza zaidi sheria za uhamiaji uliopewa jina la "Sheria ya Kupunguza Mmiminiko."
Pendekezo la Jumatano lilibua hasira kubwa nchini Ujerumani, ambako ushirikiano wowote na vyama vya siasa kali limekuwa likionekana kama jambo lisilokubalika, na AfD inatazamwa na wengi kama chama cha itikadi kali kinachovuka mipaka ya kisiasa ya kidemokrasia.
Wakosoaji wamemlaumu Merz kwa kubomoa kile wanachokiita kizuwizi dhidi ya AfD. Maelfu ya watu walifurika mitaani tena Ijumaa jioni, baada ya maandamano mengine katika miji mbalimbali Alhamisi, na maandamano zaidi yanapangwa kwa wikendi nzima kote nchini Ujerumani.