Musiala afanyiwa upasuaji baada ya kuumia vibaya
8 Julai 2025Kiungo mshambuliaji wa Bayern Munich Jamal Musiala amefanyiwa upasuaji baada ya kupata majeraha mabaya ya mguu wakati wa mashindano ya vilabu ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Marekani, taarifa hiyo imetolewa na timu yake ya Bayern Munich ambayo ndio mabingwa wa Ujerumani msimu uliomalizika.
Musiala alipata jeraha baya la goko katika mguu wake wa kushoto baada ya kugongwa na kipa wa Paris Saint-Germain Gianluigi Donnarumma mwishoni mwa kipindi cha kwanza katika mchezo wa robo fainali siku ya Jumamosi na ambao Bayern Munich walichapwa 2-0 na kutupwa nje ya mashindano hayo.
Nyota huyo wa Ujerumani mwenye miaka 22 sasa atakosa mechi za awali za ligi kuu kandanda ya Ujerumani bundesliga na zile za timu ya taifa za kufuzu kwa Kombe la Dunia zinazoanza Septemba lakini anatarajiwa kurejea dimbani mwishoni mwa mwaka huu.