Museveni mbioni kuwavutia wafuasi wa Bobi Wine
11 Agosti 2025Ijapokuwa Rais Museveni amesisitiza kuwa ziara anazozifanya mjini Kampala na katika vitongoji vyake anazotoa ruzuku za pesa kwa makundi mbalimbali si za kampeni, ni dhahiri kwamba huu ni mojawapo ya mkakati wake wa kuwavutia wapigaji kura. Anawalenga hasa watu wa tabaka la chini maarufu kama watu wa Ghetto ambao awali jamii iliwachukulia kuwa wanyonge wasiokuwa na ushawishi wowote katika siasa za nchi.
Ama baada ya jumuiya hiyo ya watu kuhamasishwa na Bobi Wine, walikuja kutambua uwezo wao katika suala zima la demokrasia na uongozi, wakashiriki katika uchaguzi kama wapigaji kura au wagombea. Awali hawakufahamu kuwa nao wanaweza kutumia majukwaa ya siasa kupata haki zao badala ya kubaki tu wakitoa vilio na miito wakitumia msemo maarufu wa ''Gavumenti etuyambe'' yaani serikali itusaidie. Hao ndiyo wamejitoa muhanga na kuendelea kumshabikia Bobi Wine, licha ya baadhi yao kukamatwa na kuhujumiwa na vyombo vya dola. Joel Senyonyi ni kiongozi wa upinzani bungeni na pia msemaji wa chama kikuu cha upinzani NUP.
Bobi Wine asema vitisho dhidi yake vimezidi kuongezeka kuelekea uchaguzi wa urais, 2026
''Museveni alipotembelea Ghetto za mtaa wa Kawempe alishangaa jinsi maisha ya watu wa Ghetto yalivyo. Alihoji kwa nini kuna Ghetto nyingi Kampala na kuuliza mnaishi hivi. Ni fedheha kubwa kwa mtu ambaye ametawala nchi kwa miaka 40 kuuliza kushangaa jinsi hiyo. Hii ina maana kuwa utawala hautambui thamani ya hao watu,'' alisema Joel Senyonyi.
Kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2021, matarajio ya raia wengi wa Uganda ni kwamba kinyang’anyiro kwa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026, kitakuwa kati ya Rais Museveni wa chama tawala cha NRM na Bobi Wine wa chama kikuu cha upinzani cha NUP. Kwa hiyo si ajabu kwamba mahasimu hao wawili wa kisiasa sasa wanapigania kura za wanaGhetto. Mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 2021, Rais Museveni alianzisha mpango maalum wa kutoa ufadhili wa kifedha na vifaa kwa makundi ya vijana wa Ghetto hasa wale wa mji wa Kampala. Katika mojawapo ya mikutano ya hadhara hivi karibuni Rais Museveni alisisitiza kuwatambua wanaGhetto.
''Hii si mara yangu ya kwanza kuja Ghetto. Mara yangu ya kwanza ilikuwa mwaka 1968. Nimewawezesha nyinyi wanaghetto kupata mafunzo ya kazi mbalimbali za mikono. Kwa hiyo nawaomba nanyi mniunge mkono kisiasa.''
Huenda Museveni anaendelea kufaulu kubadili fikra za wanaghetto
Kwa kiwango fulani Rais Museveni akitumia ushawishi mbalimbali amefaulu kuwabadili baadhi ya wanaGhetto fikra juu ya uongozi wake. Kupitia kwa vyama vya akiba na mikopo vya Ghetto alivyoanzisha mara tu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2021, kiongozi huyo anajivunia kuwa na vijana wafuasi zaidi ya elfu arobaini wa Ghetto mjini Kampala pekee ambao wanadai awali walikuwa wafuasi wa Bobi Wine.
''Idadi ya wanachama wa muundo wa Ghetto imefikia 40,000 katika mji wa Kampala pekee. Kutokana na hali hii, uhalifu umepungua kwani vijana wengi wa Ghetto wana kazi. Hata ghasia za kisiasa zimepungua mheshimiwa rais.''
Wajumbe wa NRM kuwachagua wagombea wa uchaguzi wa 2026
Lakini kwa mtazamo wa Joel Senyonyi harakati za Rais Museveni kuwashawishi watu wa Ghetto hazitabadili msimamo wao na wataendelea kuunga mkono upinzani.
''Walijaribu katika uchaguzi uliopita na hawakufaulu''
Vijana wengine wa Ghetto wanakubaliana na kauli hii. Wanadai kuwa wamendelea kunyanyaswa sana na utawala wa Rais Museveni kwa takriban miaka 40, hata akiwamiminia pesa hawatomuunga mkono kwani hizo hizo pesa ni haki yao kuzipata kwa njia nyengine akijenga mazingira yanayoboresha maisha ya watu wa Ghetto kwa kutoa huduma bora za elimu, afya na njia za kupata mitaji. Bila shaka kinyume na miaka ya nyuma, wanaGhetto wana ushawishi mkubwa kwa sasa katika siasa za Uganda.
Haya yaweza kutajwa kuwa mafanikio makubwa ya Bobi Wine na wanasiasa wenzake katika kumshinikiza Rais Museveni kiasi kwamba sasa naye anaonyesha kutaka kuvishwa taji la rais wa Ghetto. Lakini baadhi wanasisitiza kuwa rais asili na halisi wa Ghetto ni Bobi Wine. Lubega Emmanuel, DW Kampala.