Museveni atafuta suluhisho la mzozo wa Sudan Kusini
4 Aprili 2025Museveni alipokewa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Juba na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, ambaye utawala wake umemtuhumu makamu wa kwanza wa rais Riek Machar, kuchochea uasi na kumuweka katika kifungo cha nyumbani.
Kiongozi huyo wa Uganda ambae wanajeshi wake walipelekwa Sudan Kusini mwezi uliopita, kujaribu kuimarisha usalama wa mji mkuu Juba, hakuzungumzia moja kwa moja mgogoro wa taifa hilo changa duniani alipokuwa katika uwanja huo wa ndege, aliwaambia waandishi habari kwamba atafanya mazungumzo na Kiir kuhusu uhusiano na ushirikiano wa mataifa hayo mawili.
Waziri wa nchi anayehusika na masuala ya kikanda wa Uganda John Mulimba, anaeshughulikia ushirikiano wa kikanda alisema mkutano kati ya viongozi hao wawili uliendeshwa vizuri na uligusia mambo mengi ikiwemo uchumi na biashara.
"Tumekuwa na mkutano mzuri, uliogusia masuala kati ya serikali zetu ambayo ni ya manufaa kwa serikali zote. Tumegusia suala la amani na usalama kati ya nchi zetu na pia kikanda. tumejadiliana pia masuala ya biashara, uchumi na jamii”, alisema Mulimba.
Salva Kiir hata hivyo alidokeza kuwa yeye na mwenzake watajadili kuhusu hali ya sasa ya kisiasa nchini humo.
Juhudi za kimataifa
Ziara ya Museveni imejiri baada ya kufanyika juhudi za upatanishi kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC zilizofanyika wiki hii kwa lengo la kutafuta njia ya kuachiwa kwa Riek Machar ili kuzuwiya hali kuwa mbaya zaidi.
Riek Machar alikamatwa wiki iliyopita na vikosi vilivyotiifu kwa Kiir huku waangalizi wa kimataifa wakielezea wasiwasi wao wa kutokea vita vikali zaidi kati ya wanajeshi waliotiifu kwa viongozi hao wawili.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukihimiza magungumzo ya kufikia suluhu ya mvutano huo. Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga pia alikuwepo Sudan Kusini wili iliyopita alizungumza na Kiir lakini hakuweza kuzungumza na makamu wake wa rais.
Hli iliyoko sasa inachochea ukiukwaji wa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka mitano na vilivyosababisha mauaji ya watu 400,000 wa taifa hilo.
Wiki iliyopita naibu mwenyekiti wa chama cha Machar cha Sudan People's Liberation Movement In Opposition (SPLM/IO), alisema kuzuiwa kwa Machar kumefuta makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa mwaka huo wa 2018 kati ya Kiir na Mchar.