Museveni kugombea tena urais mwakani
25 Juni 2025Museveni mwenye umri wa miaka 80 ameitawala Uganda tangu mwaka 1986 ikimaanisha kuwa katika kipindi cha miaka 40 amezidi kujiimarisha hasa kupitia mabadiliko ya Katiba ambapo ukomo wa awamu mbili uliondolewa na kisha baadaye ukomo wa umri.
Wanaharakati wa haki za binadamu na wapinzani wa kisiasa wanasema Rais Museveni anaendeleza utawala wake kwa kutegemea nguvu za jeshi na vyombo vya dola kuwanyamazisha wakosoaji.
Miongoni mwa wakosoaji wake maarufu ni Dkt. Kizza Besigye, ambaye baada ya kukamatwa katika mazingira ya kutatanisha jijini Nairobi, amebaki kizuizini akikabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Besigye aendelea kuteseka kizuizini
Mkewe, Winnie Byanyima, amesema Besigye anaendelea kuteswa kwa sababu ya msimamo wake dhidi ya utawala wa kimabavu wa Museveni, na ametoa wito kwa rais huyo kumwachia huru mumewe, akisisitiza kuwa mashtaka ni ya kisiasa na mahakama hazina uhuru wa kutoa haki ya kweli kwake.
Mkuu wa uchaguzi wa chama tawala cha NRM, Tanga Odoi, ametangaza kuwa Rais Yoweri Museveni atajitokeza Jumamosi kuchukua fomu ya uteuzi kugombea tena urais kupitia chama hicho pasina mpinzani mwingine ndani ya chama.
Ingawa katika miaka ya hivi karibuni mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, aliashiria nia ya kugombea urais, alipandishwa cheo kuwa mkuu wa majeshi na akapunguza harakati hizo, japokuwa bado kuna uvumi kuwa ndiye anayetarajiwa kumrithi.
Yako wapi makabidhiano ya kidemokrasia ya mamlaka?
Waziri mkuu wa zamani, Amama Mbabazi ameonya kuwa kukosekana kwa mchakato wa amani wa kupokezana madaraka kunaweza kuiingiza Uganda katika machafuko ya kisiasa.
Katika kipindi hicho, vyombo vya dola vimeendelea kumwandama kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, huku wafuasi kadhaa wa chama chake cha NUP wakikamatwa na kuzuiliwa kwa tuhuma mbalimbali.
Mlinzi wake mkuu, Eddy Mutwe, alitoweka kwa siku kadhaa kabla ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuthibitisha kuwa alikuwa akimshikilia binafsi. Matukio haya yamezua hofu miongoni mwa raia kuhusu hali ya usalama na haki wakati wa kampeni na uchaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa Museveni anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa juu ya vyombo vya dola.
Kwa sasa Bobi Wine anahimiza wananchi kushiriki katika kile anachokitaja kuwa kura ya hasira dhidi ya Museveni ambayo lengo lake ni kupelekea matokeo ya uchaguzi huo kutokuwa halali pale wanapomkosesha ridhaa ya zaidi ya asli mia 50.