Muongozaji filamu wa Kipalestina aachiwa na Israel
26 Machi 2025Mamlaka za Israel zimemuachia huru Hamdan Ballal, muongazaji wa Kipalestina wa filamu ya "No Other Land" iliyoshinda tuzo ya Oscar, siku moja baada ya kushambuliwa na walowezi wa Kiyahudi na kisha kukamatwa na wanajeshi.
Ballal na Wapalestina wengine wawili walishutumiwa kurusha mawe dhidi ya mlowezi mmoja, madai ambayo wanayakanusha.
Wakati huo huo, bunge la Israel limepitisha bajeti muhimu ya serikali, hatua ambayo inampa nguvu zaidi Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, licha ya shinikizo kubwa la umma kutokana na vita vinavyoendelea huko Gaza.
Soma pia: Israel yatishia kuiangamiza Hamas ikiwa haitowaachia mateka
Mashambulizi ya usiku ya Israel katika ukanda huo wa Gaza yameua watu wasiopungua 23, wakiwemo watoto watatu na wazazi wao waliouawa katika hema lao. Wizara ya Afya imeripoti zaidi ya watu 792 wameuawa na wengine 1,663 kujeruhiwa ndani ya wiki moja tangu Israel ilipovunja makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas.