Muda wa kutunga katiba mpya ya Iraq umerefushwa
16 Agosti 2005Tangu mwanzo ilijulikana haitakuwa kazi rahisi kuipatia Iraq katiba, nchi ambayo ina makabila, dini na madehehebu mbali mbali ya dini. Sio rahisi kuyaweka katika chungu kimoja maslahi ya makundi yote hayo. Dimokrasia maana yake ni kuwapa madaraka walio wengi, na walio wengi huko Iraq ni Washia walio 60 asilimia ya wakaazi.. Hawa sasa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Iraq, ndio waliokamata mpinu wa kisu. Kundi la pili kwa ukubwa ni Wakurd, walio karibu asilimia 25 ya wakaazi. Nao wanataka wapewe haki ambazo hadi karibuni walikuwa wananyimwa. Wasunni hadi karibuni ndio waliokuwa watawala, na sasa, kama vile walivyo Wakristo wachache, itabidi siku za baadae kutokuwa na umuhimu wa kisiasa.
Watu waliohojiwa mjini Baghdad walisema makundi makubwa, Washia, Wasunni, Waarabu na Wakurd, ni lazima yaregeze kamba na yatafute suluhisho kwa ajili ya kuwa na muafaka kuhusu katiba. Mfanya kazi wa serekalini, Mohammed Kadham, alisema wao hawajawahi kuiona katiba katika maisha yao, na jambo hilo litakuwa bora kabisa kwa Iraq; hivyo muda utakaochukuwa kwa katiba hiyo kutungwa usiwe ni sababu. Mtu mwengine, Hamid al-Zubaidi, mfanya biashara wa mazulia, alisema sio kushindwa ikiwa katiba hiyo haijaweza kumalizika kutungwa siku ya mwisho ya jana. Wengi wa wabunge 275 wa Iraq walikubali kuurefusha muda wa kuitunga katiba hiyo hadi Agosti 22. Masuala ambayo yana utata hadi sasa katika kuikamilisha katiba hiyo yanaanzia tangu mfumo wa serekali ya shirikisho kwa Iraq, dhima ya dini ya Kiislamu katika serekali baada ya Saadam Hussein hadi namna ya kugawana mali inayotokana na hifadhi kubwa ya mafuta yalioko katika nchi hiyo, ya pili kwa wingi duniani baada ya Saudi Arabia.
Bwana Zubaidi alisema hamna katiba katika dunia ambazo hazijakuwa na tafauti na mashauriano pale zilipokuwa zinatungwa. Aliongeza kusema yeye anafikiri Wakurd wanataka mengi sana. Alisema Wakurd wanafikiri wao pekee ndio waliokandamizwa chini ya utawala wa Saadam Hussein, lakini ukweli ni kwamba Iraq nzima ilikandamizwa. Alisema, hata hivyo, anafikiri Wakurd wataregeza kamba na hawataligawa taifa.
Viongozi wa Ki-Kurd wanataka kuwa na utawala wa ndani wa eneo lao la kaskazini ya Iraq ndani ya shirikisho, eneo ambalo lina wakaazi kati ya milioini tatu hadi nne. Pia wanataka mipaka ya eneo hilo ichorwe upya kuuingiza mji wa Kirkuk ulio na utajiri wa mafuta. Mjini Baghdad, Yasser Ghazi anahisi Marekani inahitaji kujiingiza zaidi kuyafanya makundi mawili- Wakurd na Washia- watanzuwe tafauti zao. Bibi Faten Ismail anasema masuala ya upungufu wa umeme na maji ni mambo ambayo yanahitaji kutanzuliwa kwanza. Fikra zake zilikuwemo katika magazeti ya Iraq yalioonya juu ya kusambaratika huduma za kimisngi.
Naye Rais George Bush wa Marekani amezipongeza juhudi za kijasiri za Wa-Iraqi katika kukamilisha kuitunga katiba yao. Serekali ya Marekani inahitaji sana kuibakisha kasi ya kutafuta suluhisho la kikatiba ili kukabiliana na uasi ambao umesababisha vifo vya Wamarekani katika nchi hiyo kuengezeka na watu kupungua kuviunga mkono vita hivyo. Rais Bush aliwahi kunukuliwa akisema katiba ya Iraq inaweza na ni lazima ikubaliwe ifikapo Agosti 15.
Kwa mujibu wa sheria iliotungwa na Marekani kuhusu kipindi cha mpito cha utawala katika nchi hiyo, mswada wa katiba ulikuwa upigiwe kura ya maoni hapo Oktiba 15 kabla ya kufanywa chaguzi za taifa kwa ajili ya serekali ya kudumu hapo Disemba. Pindi kamati ya kikatiba itashindwa kukubaliana juu ya katiba, basi bunge la mpito litavunjwa na kutaitishwa uchaguzi wa bunge jipya, ambalo baadhi ya watu wanasema itakuwa kualika michafuko ya kisiasa. Mgogoro wa kutoafikiana juu ya katíba utakwamisha nafasi ya kuwaondosha wanajeshi 138,000 wa Kimarekani walioko Iraq, wakati ambapo Ikulu ya Marekani inabinywa ili iweke ratiba ya kuwarejesha nyumbani wanajeshi hao.
Miraji Othman