Mtaalamu wa UN: Israel inaendesha "mauaji ya kimbari" Gaza
3 Julai 2025Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maeneo yanayokaliwa kimabavu ya Wapalestina, Francesca Albanese, ameitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel vikwazo vya silaha na kusitisha ushirikiano wa kibiashara na kifedha, akidai kuwa Israel inatekeleza "kampeni ya mauaji ya kimbari” katika Ukanda wa Gaza.
Akizungumza mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Albanese amesema hali katika maeneo ya Wapalestina ni ya kutisha, na kuitaja Israel kuwa inahusika na moja ya mauaji ya kimbari ya kikatili zaidi katika historia ya hivi karibuni.
" Kuna watu na mashirika ambayo yanafaidika na ghasia, mauaji na uharibifu huko Gaza na katika maeneo mengine ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu..."
Wajumbe wa Israel hawakuhudhuria kikao hicho, kufuatia sera yao mpya ya kutoshiriki vikao vya baraza hilo wakidai lina upendeleo na pia chuki dhidi ya Wayahudi.
Hayo yanajiri wakati vifo vinaendelea kuripoti Gaza huku mazungumzo ya kusaka mpango wa kusitisha mapigano yakiendelea.