Mshukiwa wa milipuko ya mabomba ya Nord Stream akamatwa
21 Agosti 2025Taarifa za kukamatwa kwake zimethibitishwa na waendesha mashtaka wa Ujerumani.
Mshukiwa huyo aliyefahamika kama Serhii K. kwa mujibu wa sheria za faragha za Ujerumani, alikamatwa usiku wa kuamkia leo karibu na mji wa Rimini, nchini Italia.
Mabomba ya gesi ya Nord Stream yaliharibiwa na milipuko ya chini ya Bahari ya Baltiki iliyotokea Septemba 26, mwaka 2022 na kusababisha kusitishwa kwa usafirishaji wa gesi kutoka Urusi kwenda Ulaya.
Uharibifu wa mabomba hayo uliibua mvutano wa kisiasa na kiusalama barani Ulaya hasa katika muktadha wa vita vya Ukraine.
Tukio hilo lilitokea katika wakati ambapo mataifa ya Ulaya yalikuwa katika harakati za kupunguza utegemezi wao kwa nishati ya Urusi, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari 2022.