MSF yasitisha shughuli zake kambi ya Zamzam Sudan
25 Februari 2025Kundi hilo la madaktari wanaotoa misaada ya matibabu, linalojulikana pia kama MSF, limesema mapigano kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF yameongezeka ndani ya kambi hiyo ilioko eneo la kaskazini mwa Darfur.
Kupitia taarifa, MSF imeeleza kuwa, kuongezeka kwa mapigano kumefanya iwe vigumu kwao kutoa msaada wa kibinadamu kwa maelfu ya watu waliopoteza makaazi yao.
Imeongeza kuwa imesitisha shughuli zao zote, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma katika hospitali ya dharura.
Mkuu wa ujumbe wa MSF nchini Sudan Yahya Kalilah amesema hatua ya kusitisha shughuli zao katikati ya janga linalozidi kuwa baya ni uamuzi wa kuvunja moyo ila hawana budi kufanya hivyo.
Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Aprili 2023 baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na kikosi cha wanamgambo cha RSF.