Afisa wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas auwawa Gaza
27 Machi 2025Kauli iliyotolewa na kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas imearifu kuwa msemaji wake Abdu Latif al-Qanou ameuwawa katika shambulio la moja kwa moja akiwa ndani ya hema huko Jabalia. Katika shambulio jingine tofauti na hilo watu sita wa familia moja wameuwawa na wengine kadhaa ambao idadi yao haikutajwa wamejeruhiwa.
Jeshi la Israel lilisema wiki iliyopita kuwa lilimuua Mkuu wa shirika la usalama wa ndani wa Hamas Rashid Jahjouh, katika shambulio la anga. Siku kadhaa kabla, kundi la Hamas liliwataja Essam al Dalis, mkuu wa serikali ya kundi hilo katika Ukanda wa Gaza na mkuu wa wizara ya mambo ya ndani Mahmud Abu Watfa, kuwa ni miongoni mwa maafisa wake waliouwawa kwenye mashambulizi ya anga ya Israel.
Kulingana na wizara ya afya iliyo chini ya Hamas takriban watu 855 wameuwawa tangu Israel ilipoanza tena vita kwenye ukanda huo baada ya awamu ya kwanza ya kusitisha mapigano kumalizika Machi 18.
Israel inaendeleza operesheni zake Gaza wakati hivi leo bunge la nchi hiyo limepitisha sheria muhimu katika mpango wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa kuifanyia mageuzi mahakama.
Wahouthi wafanya mashambulizi dhidi ya Israel
Katika sheria hiyo mpya ambayo imekumbana na ukosoaji mkubwa, kamati ya teuzi za mahakama itapewa nafasi mbili kati ya tisa kwa wanasheria watakoteuliwa na serikali kwa kushirikiana na upande wa upinzani. Nafasi hizo kwa sasa zinashilkiliwa na chama cha wanasheria wa Israel. Wateuliwa hao wapya wa kisiasa watakuwa na kura ya turufu ya kupinga teuzi zozote katika mahakama kuu ya nchini Israel.
Katika hatua nyingine, waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran wamethibitisha kuwa wamefanya mashambulizi ya makombora yaliyoulenga uwanja wa ndege na kambi moja ya jeshi nchini Israel pamoja na meli ya kivita ya Marekani.
Msemaji wa waasi hao Yahya Sarreeth amesema kuwa, "Kikosi cha makombora kiliulenga uwanja wa ndege wa Gurion Airport katika eneo linalokaliwa kimabavu la Yafa kwa kutumia kombora la "Dhu al-Fiqar", na kilililenga pia eneo la jeshi kusini mwa Jaffa kwa kutumia kombora la balistiki. Operesheni hii imefanikiwa kutimiza kikamilifu malengo yake."
Mapema Alhamisi, kabla ya tamko la Wahouthi, jeshi la Israel lilitangaza kuwa limefanikiwa kuzuwia makombora mawili kutoka Yemen kabla ya kutua katika ardhi ya Israel. Waasi wa Kihouthi wamekuwa wakirusha makombora na droni dhidi ya Israel kama ishara ya kuonesha mshikamano na wapiganaji wa Hamas.