MSC 2025: Steinmeier awataka viongozi wa Ulaya kuwa watulivu
14 Februari 2025Majadiliano katika Mkutano wa Usalama wa Munich 2025 yanajikita katika uhusiano wa kanda ya Atlantiki, nafasi ya Ulaya duniani, na vita vya Ukraine, huku Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy wakiwa miongoni mwa washiriki wakuu.
Katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kisiasa, ikiwemo kurejea kwa Donald Trump madarakani na uchaguzi ujao wa Ujerumani, mkutano huu unatarajiwa kuathiri mustakabali wa usalama wa kimataifa.
Steinmeier: Umoja wa Ulaya lazima udumishwe
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amesisitiza kuwa mkutano huu unafanyika katika kipindi muhimu kwa Ujerumani, ikizingatiwa kuwa taifa hilo litafanya uchaguzi wa bunge katika muda wa zaidi ya wiki moja.
Steinmeier, ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha Social Democratic Party (SPD), ametaja umuhimu wa Ulaya katika siasa za Ujerumani, akisema kuwa Ulaya ina nafasi muhimu katika sera za Ujerumani na itaendelea kuwa hivyo.
Soma pia: Viongozi wa Ulaya wahimiza umoja katika kuimarisha ulinzi
Amesisitiza kuwa serikali ijayo, bila kujali muundo wake, lazima ifanye kazi kwa namna inayoheshimu na kukuza umoja wa Ulaya. Pia, Steinmeier ameukosoa utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, akisema hauthamini kanuni zilizowekwa.
"Utawala mpya wa Marekani una mtazamo tofauti wa dunia na sisi. Mtazamo ambao hauthamini kanuni zilizowekwa, ushirikiano uliokua kwa muda mrefu, na uaminifu. Hatuwezi kubadilisha hilo. Tunapaswa kulikubali na kujifunza jinsi ya kushughulikia hali hiyo."
Steinmeier amewahimiza viongozi wa Ulaya kuwa watulivu mbele ya msururu wa sera zenye mvurugano kutoka Washington tangu Trump aliporejea Ikulu ya White House.
Baerbock: Hakuna nafasi kwa Urusi kurejea G7
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, ambaye pia anahudhuria mkutano huo, amepinga pendekezo la Trump la kuirudisha Urusi katika kundi la G7, akisisitiza kuwa hakuna ushirikiano wa kawaida unaowezekana na Urusi ya Putin baada ya uvamizi wake nchini Ukraine.
Aidha, Baerbock amekosoa kauli ya Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, ambaye anadaiwa kuhimiza vyama vya siasa kushirikiana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD.
Alisisitiza kuwa wapigakura wa Ujerumani pekee ndio wanaoweza kuamua uchaguzi wa bunge la nchi hiyo.
Mvutano kati ya Ulaya na Marekani
Kwa miongo kadhaa, uhusiano wa karibu kati ya Marekani na Ulaya umekuwa msingi wa Mkutano wa Usalama wa Munich, ukijengwa juu ya ushirikiano na heshima ya pande zote.
Hata hivyo, tangu Donald Trump kurejea madarakani, uhakika huo umeanza kuyumba.
Ingawa Trump hatakuwepo mkutanoni, athari zake zitaonekana, hasa kwa viongozi wa kijeshi wa Ulaya wanaokabiliana na madai yake juu ya matumizi ya ulinzi na mpango wa amani kwa Ukraine.
Kabla ya kuanza kwa mkutano, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na Waziri wa Mambo ya Nje Annalena Baerbock walikutana na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, pamoja na mjumbe maalum wa Marekani, Richard Grenell.
Vance pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na Friedrich Merz, mgombea anayepewa nafasi kubwa kuwa Kansela wa Ujerumani baada ya uchaguzi wa Februari 23.
Kansela wa sasa, Olaf Scholz, anatarajiwa kufika Munich Jumamosi, lakini hana mpango wa kukutana na Vance.