Msamaha wa Trump: Zawadi kwa marafiki, kisasi kwa Wapinzani?
30 Mei 2025Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kutumia mamlaka ya kiutawala ya kutoa msamaha kwa njia inayowashangaza wachambuzi wa sheria na demokrasia. Katika msururu wa hivi karibuni wa waliopata msamaha, kuna wanasiasa waliowahi kufungwa kwa ufisadi, mastaa wa televisheni waliopatikana na hatia ya utapeli wa mabenki, na hata rapa maarufu aliyehusika na kesi za silaha.
Wapokeaji hao ni sehemu ya mwenendo unaozidi kujitokeza katika uongozi wa Trump — ambapo msamaha wa rais hutolewa kwa marafiki wa kisiasa na wale walio na uhusiano wa karibu na Ikulu, huku raia wa kawaida wakiendelea kupuuzwa licha ya kuwasilisha maombi yao kwa miaka mingi.
Waliopata msamaha: Washirika, wanasiasa na mastaa
Miongoni mwa waliopata msamaha wa hivi karibuni ni:
Michael Grimm, mbunge wa zamani wa Republican kutoka New York, aliyepatikana na hatia ya udanganyifu wa mapato ya mgahawa wake na kufungwa miezi nane.
John Rowland, gavana wa zamani wa Connecticut, aliyefungwa mara mbili kwa makosa ya kupokea zawadi kinyume cha sheria na kuficha kazi zake kwenye kampeni za kisiasa.
Todd na Julie Chrisley, nyota wa kipindi cha "Chrisley Knows Best", walipatikana na hatia ya kuwasilisha nyaraka bandia ili kupata mikopo ya zaidi ya dola milioni 30 na kukwepa kulipa kodi.
NBA YoungBoy, rapa maarufu aliyekabiliwa na kesi za umiliki haramu wa silaha.
Trumppia amewahi kutoa msamaha kwa washirika wake waliokumbwa na uchunguzi wa Urusi, pamoja na Charles Kushner, baba mkwe wa mwanawe Jared, aliyeteuliwa baadaye kuwa balozi wa Marekani nchini Ufaransa.
Wachambuzi wanasema Trump anatumia msamaha wa rais kama njia ya kuvunja hukumu za mahakama, kupinga waendesha mashtaka, na kutimiza malengo ya kisiasa.
Liz Oyer, aliyekuwa wakili wa wizara ya Sheria anayeshughulikia misamaha, alifutwa kazi baada ya kukataa kuidhinisha kurejeshwa kwa haki ya kumiliki bunduki kwa muigizaji Mel Gibson.
"Anatumia msamaha kama njia ya kulipa fadhila au kulipiza kisasi. Hii ni hatari kwa mfumo wetu wa haki," alisema Oyer.
Matumizi ya msamaha kwa maslahi binafsi
Tangu kurejea madarakani, Trump amevunja utaratibu wa kawaida wa kushughulikia misamaha. Badala ya kutegemea mapendekezo ya ofisi ya msamaha, aliwateua washirika wa kisiasa kama Ed Martin, ambaye sasa ameahidi kuchunguza misamaha iliyotolewa na Rais Biden kwa wanafamilia wake.
Kwa upande mwingine, wizara ya sheria imepunguza nguvu ya Kitengo cha Maadili ya Umma kilichoundwa baada ya kashfa ya Watergate ili kushughulikia kesi za matumizi mabaya ya madaraka ya umma. Idadi ya wanasheria katika kitengo hicho sasa imepungua hadi wachache mno baada ya uongozi wa juu kuingilia kesi kadhaa, ikiwemo dhidi ya Meya wa New York, Eric Adams.
Katika siku yake ya kwanza tu baada ya kurejea madarakani, Trump alitangaza msamaha au kufuta kesi za zaidi ya watu 1,500 waliokamatwa kwa kuhusika na shambulio la Capitol Januari 6, 2021 — hatua iliyotafsiriwa kama kupotosha haki na kushawishi wafuasi wake kisiasa.
"Msamaha huu unaendana na mtindo wa Trump wa kutumia mamlaka yake kama zana ya kulipa fadhila au kulipiza kisasi, badala ya kutekeleza sera kwa manufaa ya wote,” alisema Julian Zelizer, mwanahistoria wa urais kutoka Chuo Kikuu cha Princeton.
Kwa msamaha wa kisiasa unaozidi kuwa wa wazi, Trump anaweka alama ya aina yake katika historia ya urais wa Marekani — ambapo uaminifu wa kisiasa na umaarufu vinaonekana kuwa vigezo muhimu zaidi kuliko haki, toba au usawa wa kisheria.
Chanzo: AP