Msamaha kwa waasi kaskazini mwa Uganda waelekea kuzaa matunda.
27 Septemba 2004Nchini Uganda wakati vita kati ya majeshi ya serikali na waasi wa Lord Resistance army –LRA-vinaendelea, kuna mafanikio upande wa hatua ya msamaha iliotangazwa na serikali kwa waasi .Miongoni mwa waliojisalimisha na kupelekwa katika kituo maalum cha kuwarejesha katika maisha ya kawaida kinachojulikana kama World vision rehabilitaion Centre katika mji wa Gulu kaskazini mwa Uganda , ni pamoja na Jackson Acama mwenye umri wa miaka 42 ambaye anadai alikua na cheo cha Meja katika jeshi la waasi. Mafanikio hayo yanatokana na matangazo ya stesheni moja inayojulikana kama MEGA FM.
Kama walivyo waasi wengine 174, katika kituo hicho, Jackson naye pia amepewa msamaha na serikali ya Uganda. Binafsi anasema muda wote amekua akisikia juu ya msamaha , kwa njia ya redio, lakini ilikua ni mwezi Aprili mwaka huu, ambapo aliweza kufanya matayarisho pamoja na majeshi ya serikali kumrudisha nyumbani kwa ndege kutoka nchi jirani ya Sudan, ambako bado kuna wengi miongoni mwa waasi wa LRA.
Katika miaka ya karibuni, uhusiano wa vuta nikuvute kati ya Uganda na Sudan, uliwapa hakikisho waasi wa LRA kuendesha harakati zao kutokea Sudan na Uganda nayo ikashutumiwa kuwaunga mkono waasi wa kusini mwa Sudan wa SPLA.Hata hivyo mazungumzo ya amani baina ya maafisa wa Sudan na SPLA yamesaidia kurekebisha uhusiano wa nchi hizo mbili.Ingawa Uganda haijaanza mazungumzo rasmi na waasi wa LRA, kujisalimisha kwa waasi kama Jackson Acama kunaweza pia kua ishara kwamba vita vya miaka 17 nchini Uganda navyo vinakaribia kumalizika.
Msamaha wa serikali ulitangazwa mwaka 2000. Hadi Aprili mwaka huu zaidi ya waasi 6,500 wamejitokeza kutoka msituni, kujiunga na hatua hiyo, huku 823 wakisaini msamaha huo baina ya Juni na Agosti mwaka huu. Kamanda wa majeshi ya serikali Nathan Mugisha anasema kwa wastani waasi 10 hujisalimisha kila siku katika kambi ya kijeshi ya Gulu."Hawana makao, wana randa randa tu wakiwa na njaa na bila chakula .Hivyo kila siku wanalihama jeshi la waasi"-Aliongeza kamanda Mugisha.
Wengi wa waasi hupata habari kuhusu msamaha wa serikali kupitia Redio maalum ya FM inayojulikana kama MEGA FM. Stesheni hii ya redio iliogeuka kuwa maarufu mno kaskazini mwa Uganda husikika katika eneo hilo zima na kuna kipindi maalum cha mara tatu kwa wiki kwa lugha ya Acholi.kabila kuu katika eneo hilo. Kipindi hicho huitwa Dwogpaco yaani Karibuni tena nyumbani na husikika pia kupitia matangazo ya Redio Juba kusini mwa Sudan. Redio MEGA-FM imefanikiwa kuwafanya waasi kuelewa maana halisi ya msamaha . Mbali na kipindi hicho kuna kipindi cha mjadala wa kisiasa ambacho baadhi ya wakati hupokea hata simu kutoka kwa makamanda wa LRA walioko msituni akiwemo Kiongozi wao Joseph Kony.
Kama mbinu ya kusaka njia ya maelewano katika juhudi za kumaliza vita hivyo, maafisa wa MEGA FM wanasema, kinachowasaidia ni kuwa hawaelemei upande wowote bali ni mchango katika kuleta ufumbuzi chini ya usemi-kama waasi wanaiamini redio hiyo, basi serikali nayo haina budi kuitumia kuwafikia waasi, ingawa kuna wasiotaka kuusikia ujumbe huo.
Waasi wa LRA wamekua wakiendesha vitendo vya kinyama kuanzia mauaji ya raia hadi, kuwateka nyara watoto wa Kiacholi na kuwatumia kama wapiganaji au kwa ngono.
Shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto liliripoti karibuni kwamba watoto 12,000 wametekwa nyara tokea Juni 2002 na zaidi ya 20,000 baina ya 1986 na 2004. Ingawa wengi wamerejea nyumbani miaka ya karibuni lakini bado kuna wengi waliotoweka. Kiongozi wa waasi Joseph Kony ambaye ni kutoka kabila la Acholi anajitaja kuwa ni nabii na lengo lake ni kuiona Uganda ikifuata amri 10 za Biblia. Anadai kuwa amejiwa na ndoto kuwa siku moja LRA itaongozwa na mtoto mdogo. Waasi mara nyingi hulazimishwa kufanya mauaji na mara nyengine kuwauwa hata jamaa wa waasi katika maeneo ya karibu.
Wale wanaofanikiwa kutoroka na kujisalimisha, huwekwa katika kituo maalum cha World Vision, ambako mbali na kupatiwa elimu ya kurejea katika maisha ya kawaida, lakini maafisa husaidia kuzisaka familia zao, ili waweze kujiunga tena na jamaa zao, na kufanyiwa taratibu za kijadi za msamaha za kabila la Acholi.Pamoja na hayo Acama anahofia kwamba kutokana na uhaba wa nyezo za kutosha kuweza kuwasaidia waaasi hao wa zamani, pamoja na umasikini na matatizo ya kuwapatia makaazi mapya, ni mambo yanayoweza kuwarudisha tena katika kundi la LRA. Muhimu ni ardhi.
Wakati jeshi la Uganda lilikosea mara kadhaa kumtia nguvuni Kony katika mashambulio ya Julai mwaka huu katika makao yake kusini mwa Sudan, waasi wameendelea kufanya hujuma za mara kwa mara, lakini jeshi la serikali linadai idadi yao imepungua hadi karibu 500 wakitawanyika kaskazini mwa Uganda na kusini mwa Sudan