Mpinzani wa Erdogan Imamoglu achaguliwa kugombea urais
24 Machi 2025Meya wa Istanbul, Ekrem İmamoğlu, ameteuliwa rasmi kuwa mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki (CHP) jana Jumapili, licha ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu mapema siku hiyo, akishtakiwa kwa tuhuma za rushwa na ugaidi, ambazo amezikanusha vikali.
İmamoğlu alipata kura nyingi kutoka kwa wanachama milioni 1.6 wa chama chake, huku pia akipata zaidi ya kura milioni 13 za ishara kutoka kwa raia wengine wa Uturuki, jambo lililoonyesha umaarufu wake mkubwa kama mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdoğan.
Soma pia: Erdogan asema hatosalimu amri kwa vitisho vya ghasia Uturuki
Kukamatwa kwake kumezua maandamano makubwa ya nchi nzima kwa usiku tano mfululizo, ambapo mamia ya maelfu ya watu wamejitokeza kupinga hatua hiyo na kudai aachiliwe, wakiikosoa serikali ya Erdoğan kwa kutumia kesi hiyo kisiasa ili kumzuia mpinzani mwenye nguvu.
Hata hivyo, uwezekano wa kugombea kwake urais bado haujulikani, kwani uteuzi wake rasmi utahitaji kuidhinishwa na tume ya uchaguzi nchini humo, ambayo kwa sasa inaaminika kuiunga mkono serikali.