Mpango wa Marekani juu ya misaada ya kiutu Gaza wapingwa
9 Mei 2025Katika taarifa iliyotumwa kupitia Telegram, kundi hilo limesema wapiganaji wake walifanya shambulio la uvamizi dhidi wanajeshi 12 wa Israel katika mtaa wa Tanur kwa kutumia makombora ya kushambulia magari ya kivita.
Jeshi la Israel baadaye lilithibitisha kuwa wanajeshi wake wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa vibaya.
Hili ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kuripotiwa Rafah katika wiki za hivi karibuni, eneo ambako jeshi la Israel limeongeza operesheni zake kufuatia kuvunjika kwa mpango wa kusitisha mapigano wa wiki sita uliofadhiliwa na Marekani mwezi Machi.
Licha ya utulivu wa awali, mashambulizi ya Alhamisi yanaonesha kurejea kwa mwelekeo mkali wa vita ambavyo sasa vimeendelea kwa zaidi ya miezi 19.
Pendekezo la Marekani kuhusu misaada ya kiutu Gaza lakosolewa
Wakati mapigano yakiendelea, Marekani imetangaza kuanzishwa kwa mfumo mpya wa usambazaji wa misaada kwa wakazi wa Gaza, ambao hautaihusisha Hamas wala Israel moja kwa moja.
Balozi wa Marekani nchini Israel, Mike Huckabee, amesema mfumo huo utaongozwa na mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wa kimataifa, huku Israel ikihusika tu kutoa ulinzi wa kijeshi kwa ajili ya usalama wa wasambazaji wa misaada.
"Kuna vipengele muhimu ambavyo rais amevitaka vizingatiwe tunapoanza mchakato huu. Kwanza, chakula kisambazwe kwa ufanisi, lakini pia kwa usalama ndani ya Gaza kwa watu wanaokihitaji sana. Na pili, jambo hili muhimu lifanyike kwa namna ambayo Hamas haitafaidika kwa namna yoyote." amesema Mwanadiplomasia huyo.
Hata hivyo, mpango huo umekosolewa vikali. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumiwa watoto UNICEF, na Shirika la Msaada kwa Wakimbizi wakipalestina UNRWA, na mengine ya misaada ya kibinadamu yamekemea hatua ya kuupuuza Umoja wa Mataifa katika usambazaji wa misaada.
Shirika la UNRWA, lenye wafanyakazi zaidi ya 10,000 ndani ya Gaza, limesema haiwezekani kusambaza misaada bila wao kutokana na uwezo na miundombinu waliyonayo.
Wakosoaji wanasema mpango huo unaweza kuongeza mateso kwa raia na kuwaweka hatarini wanapolazimika kusafiri hadi maeneo ya kijeshi kutafuta misaada.
Shirika la Gaza Humanitarian Foundation, linaloaminika kuwa sehemu ya mpango huo mpya unaoungwa mkono na Marekani, linaripotiwa kuanzisha "vituo salama vya usambazaji" vinavyotarajiwa kuhudumia hadi watu milioni moja kwa awamu ya kwanza.
Hata hivyo, maafisa wa misaada wanasema vituo hivyo vinaweza kulazimisha Wapalestina waliokimbia makazi kuchagua kati ya kufa au kuhamishwa tena, hasa wakati Israel inaendelea na mashambulizi katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa Gaza.
Juhudi za kidiplomasia ´zaingia ganzi´ mzozo wa Gaza
Wakati huo huo, juhudi za kidiplomasia kurejesha usitishaji mapigano bado zimekwama.
Hamas imetoa pendekezo la kuwaachia mateka wote endapo Israel itajiondoa kabisa kutoka Gaza—pendekezo ambalo Israel imelipinga.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameonesha matumaini ya kupatikana kwa makubaliano mapya ya amani na amezungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu suala la mateka na hali ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa taarifa za Israel, shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023 liliua watu 1,200 na watu 251 walichukuliwa mateka.
Kwa upande mwingine, mashambulizi ya Israel yameripotiwa kuua zaidi ya Wapalestina 52,000, wengi wao wakiwa raia, kwa mujibu wa mamlaka ya afya inayoendeshwa na Hamas.
Mashirika ya misaada yanatoa wito wa kuondolewa kwa vizuizi vya misaada na kurudi kwenye mfumo wa haki, usioegemea upande wowote, ili kuzuia baa la njaa linaloonekana kujitokeza katika Ukanda wa Gaza.