Mpango wa Israel kuikalia tena Gaza wapingwa kimataifa
5 Mei 2025Baraza la Mawaziri la Israel limeidhinisha mapema Jumatatu asubuhi mpango huo, ikiwa ni saa chache baada ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Eyal Zamir kutangaza kuwa serikali imeamuru kuitwa kazini maelfu ya askari wa akiba kwa dhima ya kuimarisha na kutanua operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza.
Maafisa kadhaa waandamizi wanasema mpango huo unalenga kuisaidia Israel kufikia malengo yake ya vita ambayo ni kuwashinda na kuwatokomeza kabisa wanamgambo wa Hamas na kuwakomboa mateka waliosalia. Itakumbukwa kuwa Israel ilijiondoa Gaza mwaka 2005 baada ya kulikalia eneo hilo kwa miongo kadhaa.
Lakini kulingana na mpango huo mpya, maelfu ya Wapalestina wametakiwa kuhamia eneo la Kusini mwa Gaza, hatua inayochukuliwa kama kulazimishwa tena kuyahama makazi yao na hivyo kupelekea hali ya kibinaadamu kuwa mbaya zaidi.
Mashirika ya misaada yapinga hatua hiyo ya Israel
Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) Jan Egeland ameupinga mpango huo wa Israel ambao utaitaka nchi hiyo kusimamia usambazaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza na kuutaja kuwa kinyume na kanuni za kibinadamu:
"Tulichosikia kutoka kwa Israeli ni kwamba watatumia misaada kama ngao ya kisiasa, kijeshi na udanganyifu, kwa kuruhusu tu misaada kwa vituo vichache vilivyopo kusini. Mpango ambao watu watachunguzwa, na mfumo usioweza kufanya kazi utawalazimisha watu kuhama ili kupata misaada, jambo ambalo litaendeleza njaa kwa raia."
Soma pia: Israel yaidhinisha utanuzi wa operesheni ya kijeshi Gaza
Vyanzo vilivyokaribu na wizara ya ulinzi na ambavyo havikutaka kutajwa jina, vimeeleza kuwa mpango huo utaanza kutekelezwa baada ya kumalizika kwa ziara ya Rais wa Marekani Donald Trump kwenye kanda ya Mashariki ya Kati, ziara inayotarajiwa kuanza wiki ijayo, na kuongeza kuwa hilo linatoa uwezekano kwamba huenda Israel ikakubali wakati huo mpango wa kusitisha mapigano.
Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanatilia mashaka mpango huo wakisema uwezekano wa Israel kulidhibiti na kulikalia tena kwa mabavu eneo la Gaza kwa muda usiojulikana si tu utafifiza matumaini ya kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina, lakini itakuwa changamoto kubwa kwa viongozi wa Israel kulitawala eneo ambalo watu wake wana uhasama na chuki kwao.
Pingamizi la mataifa mbalimbali duniani
Mataifa mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya yamekosoa hatua hiyo ya Israel kutaka kulitwaa eneo la Gaza. Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema tangazo la Israel linazusha wasiwasi na kusisitiza kuwa Ukanda wa Gaza ni wa Wapalestina.
Amezitaka pande zote kuelekeza nguvu kwenye mazungumzo ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka, akikumbushia uamuzi wa mwaka 2023 wa nchi za G7 ikiwa ni pamoja na Marekani, Ujerumani na Ufaransa ambao uliweka wazi kwamba unapinga kwa nguvu zote kitendo cha ukaliaji, ukoloni na kumeguliwa kwa eneo la Gaza.
(Vyanzo: Mashirika)