Mpango wa AGOA na hatma ya ajira kwa Wakenya
1 Aprili 2025Mkataba huo umekuwa kiini cha biashara kati ya Afrika na Marekani, lakini kukamilika kwake kunaweza kuathiri sekta ya viwanda na ajira nchini Kenya. Shisia Wasilwa na kina cha taarifa hiyo.
Mkataba wa AGOA umewezesha viwanda kama Ariel kilichoko jimbo la Machakos nchini Kenya kuwaajiri wafanyakazi wengi kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa zake katika soko la Marekani.
Kukamilika kwa mkataba huu kunaweza kusababisha kupungua kwa oda za mauzo kwa sababu ya ushuru mpya, jambo linaloweza kulazimisha kiwanda kupunguza idadi ya wafanyakazi au kufungwa kabisa ama kupotea kwa fursa za ajira kwa vijana na wanawake, ambao kwa sasa wanategemea sekta hii kwa riziki yao.
Soma pia:Uganda yapinga kuondolewa AGOA
Pankaj Bedi ni afisa mkuu Mtendaji wa kiwanda hiki cha Ariel. Mbali na kuhofia kukamilika kwa mkataba wa AGOA, anahofia sera mpya za rais Trump wa Marekani ambaye amekuwa akifunga mashirika yanayofadhiliwa na taifa hilo kubwa kiuchumi kama USAID, suala ambalo huenda likawaathiri.
"Kulikuwa na ukosefu mkubwa wa ajira lakini sasa tumeleta mabadiliko katika jamii hii. Idadi ya watu 150 elfu wanatutegemea moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja, hali ambayo imeleta udhabiti katika eneo hili.”
AGOA inachangia kukua kwa uchumi wa Kenya
Kwa miaka mingi, mkataba wa AGOA umechangia ukuaji wa uchumi wa Kenya kupitia sekta ya viwanda. Hata hivyo, bila AGOA, wataalam wanasema kuwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi yatapungua, jambo linaloweza kuathiri thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani.
Aidha kusambaratika kwa sekta ya viwanda kutachangia ukosefu wa ajira, jambo ambalo linaweza kusababisha changamoto za kijamii kama ongezeko la uhalifu na umasikini, kama anavyosema mwakilishi wa wafanyikazi wa kiwanda hiki cha Ariel, Norah Nasimiyu.
"Kina mama wengi sana wanafanya kazi hapa, wanafurahia sababu wanapata riziki yao hapa. Jamii kwa ujumla inafurahia sababu viwango vya uhalifu vimepungua, sababu wengi wameajiriwa hapa.”
Soma pia:Afrika yaitaka Marekani kurefusha mkataba wa AGOA
Hata hivyo wataalamu wanasema kuwa Ili kupunguza athari za kukamilika kwa mkataba wa AGOA, kiwanda cha Ariel na serikali ya Kenya inapaswa kutafuta fursa zilizoko nchini na kuwekeza kwenye viwanda. James Mwangi ni Afisa Mkuu wa Benki ya Equity.
Aidha wataalamu wanahoji kuwa Serikali inaweza kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu makubaliano mapya ya kibiashara ambayo yanaweza kusaidia sekta ya viwanda kuendelea kunufaika.
Mkataba wa AGOA ulitiwa sahihi mwaka 2000 na Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton. Lengo lake lilikuwa kusaidia nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata upendeleo wa kibiashara kwa kuuza bidhaa zao Marekani bila ushuru.