Mpaka wa Kongo-Rwanda wafungwa, M23 wakiingia Goma
28 Januari 2025Mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) karibu na mji wa Goma uliojaa majeshiumefungwa Jumatatu, chanzo kutoka ubalozi wa Ulaya na mashahidi walisema, saa chache baada ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda kuingia mji huo mkuu wa mkoa wa Kongo Mashariki. Rwanda imekana kuhusika licha ya ripoti za kuaminika kutoka Umoja wa Mataifa kuonyesha kuwa inawaunga mkono waasi wa M23.
"Mpaka umefungwa," kilisema chanzo cha ubalozi katika mazungumzo na shirika la habari la AFP. "Hakuna anayekuja, hakuna anayekondoka, isipokuwa baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na familia zao waliohamishwa asubuhi hii," alisema mfanyakazi wa misaada katika kivuko kikuu cha mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Waasi pia wameufunga uwanja wa ndege wa Goma na kuchukua udhibiti wa kituo cha redio cha serikali kilichokuwa kikiendelea kucheza muziki. Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa, Bintou Keita, alikiambia kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumapili usiku kwamba "tumekwama," huku uwanja wa ndege ukiwa umefungwa na barabara zote zimefungwa.
Machafuko Goma
Jumatatu asubuhi, kulikuwa na ripoti kuwa maelfu ya wafungwa walitoroka baada ya jela kuu ya Goma kuvunjwa. Uporaji na milipuko ya silaha ilisikiwa huku wakazi wakikimbia au kujificha ndani.
Soma pia: Waasi wa M23 waingia Goma
Baadhi ya wanajeshi wa Kongo walijisalimisha kwa vikosi vya ulinzi vya Umoja wa Mataifa baada ya muda wa mwisho wa waasi wa M23, huku wengine wakikimbia kwa mashua kuvuka Ziwa Kivu kuelekea Bukavu. Wengi wa wapiganaji wa kigeni kutoka Romania na Bulgaria waliokuwa wakipigana upande wa jeshi la Kongo walifanikiwa kuondoka Goma katika dakika za mwisho. Baadhi yao wamekabidhi silaha zao kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa.
Waasi wa M23 sasa wanafanya upekuzi katika nyumba na hoteli ili kuangalia kama kuna wanajeshi waliojificha huko.
"Ninaogopa mauaji ya kimbari yanaweza kutokea watakapofika. Mahali ambapo M23 tayari imechukua vijiji, wamewaua vijana," Paul Buyana aliiambia DW siku moja kabla ya kundi hilo la waasi kuchukua udhibiti wa Goma.
Kilichoongeza wasiwasi kwa mwanaume huyu mwenye umri wa miaka 27 kutoka Kongo ni kushindwa kwake kupata kazi, kwani wamiliki wa biashara wanahofu ya wapiganaji au waporaji waliokuwa wakifyatua risasi mjini.
Kazi ya mwisho ya Buyana ilikuwa wiki moja iliyopita, akihesabu makasha kwa mmiliki wa duka na kuyaandika kwenye orodha. Jioni hiyo, aliweza kula chakula cha jioni kikamilifu.
Bei za chakula zimepanda sana. Passy Mubalama, mtaalamu wa haki za binadamu huko Goma, alisema hivi karibuni alilipa faranga 1,000 za Kongo (karibu €0.35, $0.36) kwa ndoo ya sombe, mboga maarufu ya majani. Kwa kawaida, alikua analipa senti chache kwa kiasi hicho.
Soma pia: Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wasogezwa hadi Jumapili
Goma iko gizani kwa sababu mapigano yameharibu njia kuu ya umeme. Ni wale tu wanaotumia jenereta na wanaoweza kumudu dizeli ndio wanapata umeme na wanaweza kuchaji simu zao na kompyuta. Taa za jua sasa zinauzwa kwa faranga 60,000 za Kongo.
Kwa bei hizi, watu hawawezi tena kuweka akiba, alisema Mubalama, ingawa ni muhimu wakati wa vita. Haijulikani vita vitadumu kwa muda gani, aliongeza, na hakuna anayekwenda sokoni kununua chakula katika hali kama hii.
Hakuna mwisho wa mateso
Tangu Januari, vita vimewahamisha watu 400,000 kutoka vijijini mwao. Karibu nusu ya idadi ya watu wa Kivu Kaskazini sasa wanaishi na familia za wahisani au katika kambi.
Mmoja wao ni Pacifique Maombi. Alikimbia pamoja na familia yake ya watoto wanne na mume wake kutokana na machafuko yaliyotokea Sake. Alipoteza karibu kila kitu - nyumba yake na kazi yake kama muuguzi katika kituo cha afya. Lakini anashikilia kitu kinachompa matumaini: ushirika wa akiba.
Maombi anongoza kundi la wanawake 30 katika kambi ya wakimbizi kilomita 10 kutoka Goma. Wanawake hao huchangia kiasi kidogo kila wiki katika mfuko wa pamoja, ambako wanapatiwa mikopo kuwasaidia kuanzisha biashara ndogo.
Mateso ya wananchi ni jambo moja, lakini heshima yao ni jambo lingine. Kwa Zola Lutundula, mwalimu anayekaribisha familia nne, sehemu mbaya zaidi ni "aibu kwamba jeshi letu lilishindwa kulinda mji. Hii ni mbaya kwa sisi sote, kwa watu wote," alisema Lutundula.
Soma pia: Tshisekedi aitisha vikao vya usalama kutathmini vita
Kundi la waasi la M23,ni mojawapo ya makundi zaidi ya 100 ya silaha yanayowania udhibiti katika mkoa wenye madini katika mzozo wa miaka mingi. Kwa mujibu wa serikali ya Kongo na wataalamu wa Umoja wa Mataifa, waasi waliikalia Goma kwa muda mnamo 2012 na walijitokeza tena mwishoni mwa 2021, wakiwa na msaada mkubwa kutoka Rwanda. Rwanda imekana msaada huo.
Wachambuzi wametahadharisha kwamba kuzorota kwa usalama kunaweza kuendelea kusababisha machafuko katika eneo hilo, ambalo tayari linakabiliwa na moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, na zaidi ya watu milioni 6 wakiwa wameshuhudia uhamishaji.