Moto wa msitu wasababisha uharibifu usio kifani Korea Kusini
26 Machi 2025Nchini Korea Kusini, moto mkubwa wa misituni unaoendelea kwa siku ya tano mfululizo katika maeneo ya kusini mashariki umesababisha vifo vya watu 18 huku maelfu wakilazimika kukimbia makazi yao. Rais wa mpito wa nchi hiyo, Han Duck-soo, amesema leo kuwa moto huo umeleta "uharibifu mkubwa usio wa kawaida" na kuzidi makadirio yote yaliyofanywa awali.
Zaidi ya ekari elfu 43 za ardhi zimeteketea, majengo zaidi ya mia mbili yameharibiwa ikiwemo hekalu la kale lenye umri wa miaka 1,300 pamoja na viwanda na magari mengi. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni miji ya Andong, Uiseong, Sancheong na Ulsan.
Zaidi ya wazima moto elfu tisa, helikopta mia moja na thelathini na mamia ya magari wanaendelea kupambana na moto huo licha ya hali ya hewa kavu na upepo mkali unaozuia juhudi zao. Serikali imesema bado moto huo haujadhibitiwa kikamilifu.