Moto na Ghadhabu: Vita vikali vya Goma, DRC
13 Februari 2025Waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda waliidhibiti Minova, bandari muhimu katika Ziwa Kivu, na kuzunguka Goma yenye wakazi takribani milioni moja pamoja na maelfu waliokimbia mapigano. Kufikia Januari 23, eneo la Sake lilikuwa kikwazo cha mwisho kuelekea Goma.
Hali hii ilisababisha helikopta za jeshi la Kongo kufanya mashambulizi ya angani huku majeshi ya Kongo na wanamgambo wa eneo hilo wakijaribu kukabiliana na uvamizi huu kwa msaada wa askari wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Hata hivyo, ulinzi wa Goma ulizidi kudhoofika kutokana na mafunzo na silaha bora za M23 na jeshi la Rwanda.
Mnamo Januari 26, Goma ilishtuka kwa milio ya mabomu huku vikosi vya Rwanda vikivuka mpaka na kuushambulia mji huo, na kuwashangaza wanajeshi wa Kongo pamoja na mamluki wa Romania.
Vita vilienea hadi katika vitongoji vya mji, na kusababisha maelfu ya raia kujificha ndani ya nyumba zao. Kufikia Januari 27, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya wafungwa katika gereza la Goma kuvunja milango na kuanzisha mashambulizi, huku baadhi yao wakifa kwa kukosa njia za kutoroka.
Soma pia: Kongo yaitaka Rwanda kulipa fidia ya vita iliyosababisha
Jeshi la Kongo lilionekana kuwa halina uwezo wa kupambana baada ya maafisa wake wakuu kukimbia usiku kwa njia ya Ziwa Kivu, na kuacha askari wa kawaida wakihangaika mitaani kutafuta njia za kutoroka.
Licha ya jitihada za baadhi ya vikosi vya Kongo kupambana, ikiwa ni pamoja na kushambulia mji wa Gisenyi nchini Rwanda, vikosi vya Rwanda vilijibu kwa mashambulizi makali.
Hatimaye, Goma ilianguka rasmi mnamo Januari 28, huku waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda wakianza kusaka mabaki ya upinzani mtaa kwa mtaa. Maelfu ya wanajeshi wa Kongo walikimbilia kambi za Umoja wa Mataifa kutafuta hifadhi, na kuacha vifaa vyao vya kijeshi ovyo mitaani.
Hatima ya raia na mgogoro wa kibinadamu
Takribani watu 110,000 wamekwama mashariki mwa Kongo baada ya waasi wa M23 kufunga kambi za wakimbizi, hali iliyosababisha ongezeko la ukosefu wa makaazi na mahitaji ya kibinadamu.
Waasi hao waliwapa wakimbizi muda wa saa 72 kuondoka kwenye makambi yao, jambo lililozua taharuki miongoni mwa mashirika ya misaada.
Ingawa M23 walisisitiza kuwa kurudi makwao ni kwa hiari, Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa zaidi ya watu 110,000 wamehamia vijiji vya mbali ambavyo viko nje ya uwezo wa kufikiwa na misaada ya kibinadamu.
Soma pia: Kongo yapiga marufuku ndege zote zilizosajiliwa Rwanda kutumia anga yake
Kwa mujibu wa vyanzo vya serikali ya Kongo, watu zaidi ya 2,000 wameuawa kutokana na mapigano haya, huku hospitali zikifurika majeruhi na maiti kujaa mitaani.
Goma ilikuwa na karibu watu milioni moja waliokimbia vita kabla ya kuzidi kwa machafuko mwishoni mwa Februari, hali inayoifanya kuwa moja ya maeneo yenye mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Licha ya M23 kutangaza kusitisha mapigano kwa hiari, ripoti zinaonyesha kuwa bado kuna mapigano kati yao na jeshi la Kongo, hasa katika mwelekeo wa Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.
Waasi hao wametishia kuingilia kati ikiwa mauaji wanayodai kufanywa dhidi ya raia yataendelea.
Mustakabali wa Goma na DRC
Kuanguka kwa Goma mikononi mwa waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda ni pigo kubwa kwa serikali ya DRC na kunaashiria changamoto kubwa kwa usalama wa eneo hili.
Mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa hali inaweza kuzorota zaidi ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Swali linabaki, je, jumuiya ya kimataifa itafanya nini kusaidia kurejesha amani mashariki mwa DRC?