Morice Abraham asaini Simba kwa mkataba wa miaka miwili
31 Julai 2025Klabu ya Simba imeeleza kwamba kiungo huyo aliporejea nchini Tanzania kutokea Serbia alifanya mazoezi na Wekundu wa Msimbazi ambapo benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu Fadlu Davids walimpitisha na kumsajili moja kwa moja.
Itakumbukwa kwamba Morice alikulia katika kituo cha kukuzia vipaji cha Alliance Academy cha jijini Mwanza na aliwahi pia kuwa nahodha wa timu ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ''Serengeti Boys'' kilichoshiriki michuano ya AFCON mwaka 2019.
Morice atajiunga na kikosi cha Simba kilichopo kambini nchini Misri muda wowote mara baada ya kukamilika kwa vibali vyake vya usafiri.
Morice anakuwa miongoni mwa wachezaji watatu wapya waliosajiliwa na Simba kuelekea msimu wa mwaka 2025/26. Wengine ni kiungo mshambuliaji raia wa Senegal Allasane Kante na beki Rushine De Reuck kutoka Afrika Kusini.