Monaco yamuwania Ter Stegen
27 Juni 2025Bado haiko wazi ikiwa Marc-André ter Stegen, anayekipiga na Mabingwa wa Ligi ya Uhispania Barcelona, atabakia na kikosi hicho au la.
Gazeti la Uhispania Mundo Deportivo lilisema kuwa klabu ya Monaco inayocheza Ligi ya Ufaransa imewahi kuwasiliana na uongozi wa Ter Stegen ili kujadiliana kuhusu uwezekano wa uhamisho.
Monaco pia wameripotiwa kuelekeza macho yao kwa Paul Pogba, ambaye marufuku ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli imekwisha, na mchezaji wa zamani wa Barcelona Ansu Fati.
Ter Stegen ana mkataba na Barcelona hadi 2033
Ter Stegen, 33, amekuwa Barcelona tangu 2014 na ana mkataba hadi 2033.
Lakini timu hiyo wiki iliyopita ilimsajili Joan García kutoka kwa mahasimu wao wakubwa Espanyol, ambaye huenda akachukua nafasi ya mlinda lango namba moja wa Barcelona.
Ter Stegen, ambaye kwa muda mrefu alikuwa "benchi" kwenye msimu uliopita kutokana na maumivu makali ya jeraha la goti, amesema anataka kusalia Barcelona.
Lakini klabu hiyo pengine haitataka kumbakisha mlinda lango huyo ghali ambaye amekuwa katika orodha ya wachezaji wa akiba, huku ikiwa na walinda lango wengine Wojciech Szczesny na Inaki Peña.
Klabu ya Galatasaray ya Uturuki pamoja na Chelsea na Manchester City za England pia zimeonyesha nia ya kumsajili Ter Stegen.