MMUAGIKO MPYA WA DAMU-IRAQ:
23 Desemba 2003BAGHDAD: Wanajeshi wawili wa Marekani na mkalimali mmoja wa Kiiraqi wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea kando ya barabara mjini Baghdad.Kwa mujibu wa duru za kijeshi za Marekani,bomu liliripuka kando ya barabara ulipopita msafara wa magari ya kijeshi.Hivi ni vifo vya mwanzo kutokea tangu siku tano.Na kwa mujibu wa duru za polisi,katika mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq mtu asiejulikana amempiga risasi na kumuua jaji mmoja wa Kikurd.Kwa wakati huo huo msako wa wanamgambo ukizidi kuimarishwa,msemaji wa jeshi la Marekani amearifu kuwa Jemadari mkuu wa zamani katika idara ya usalama ya Saddam Hussein amekamatwa mjini Baquba kiasi ya kilomoita 65 kaskazini mwa Baghdad.Na vile vile wamekamatwa wanamgambo watatu wa kiislamu waliokuwa na uhusiano pamoja na Izzat Ibrahim al-Douri aliekuwa msaidizi mkuu wa Saddam Hussein.Katika orodha ya Wairaqi 55 wanaosakwa na Marekani,al-Douri ni namba sita. Kuna zawadi ya Dola milioni 10 kwa ye yote yule atakaetoa habari zitakazomkamatisha msaidizi huyo wa zamani wa Saddam Hussein.Inaaminiwa kuwa al-Douri ndio huongoza upinzani dhidi ya Wamarekani nchini Iraq.