Guterres asema Gaza imegeuka uwanja wa mauaji
9 Aprili 2025Guterres amewaambia waandishi habari kuwa mwezi mzima umemalizika bila ya msaada kuingizwa Gaza. Amesema hakuna chakula, mafuta, dawa na bidhaa za biashara.
Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel Oren Marmorstein amepinga tuhuma hizo akisema hakuna uhaba wa msaada wa kiutu katika Ukanda wa Gaza. Amedai kuwa Hamas imetumia msaada wa karibuni ulioingizwa Gaza kujenga upya nguvu zao za kijeshi.
Huku akitaja mikataba ya Geneva inayowalinda watu walioko vitani, Guterres amesisitiza wajibu wa "upande unaoikalia ardhi ya mwingine" kuhakikisha chakula na bidhaa za matibabu zinawafikia wakaazi.
Guterres pia alirejelea mapendekezo ya hivi karibuni ya Israel juu ya kudhibiti misaada inaoingizwa huko Gaza, ambayo chanzo kimoja kililiambia shirika la habari la AFP ni pamoja na kufuatilia vyakula ili kuzuia matumizi mabaya ya Hamas.
"Niseme wazi -- hatutashiriki katika mpangilio wowote ambao hauheshimu kikamilifu kanuni za kibinadamu -- ubinadamu, kutopendelea, uhuru na kutoegemea upande wowote," Guterres alisema, akitaka ziwekwe dhamana za upelekwaji wa bila vikwazo wa msaada katika eneo la pwani.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia aligusia hali ilivyo katika Ukingo wa Magharibi. "Njia ya sasa imefika mwisho -- haiwezi kuvumilika kabisa mbele ya sheria na historia ya kimataifa," alisema.
"Na kitisho cha Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kubadilika na kuwa Gaza nyingine kinafanya hali kuwa mbaya zaidi.
"Ni wakati wa kukomesha udhalilishaji, kulinda raia, kuwaachilia mateka, kuhakikisha kuna msaada wa kuokoa maisha, na kufikia makubaliano mapya ya usitishaji mapigano."
Siku ya Jumanne, Watu wasiopungua 58 waliuwawa katika mashambulizi yaliyofanywa na Israel katika kipindi cha saa 48 kwenye Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi ya Israeli usiku kucha yalisababisha vifo vya watu 19, wakiwemo watoto watano ambao nyumba yao katikati ya mji wa Deir al-Balah ililengwa, kulingana na shirika la Ulinzi wa Raia linaloendeshwa na Hamas.
Watu wengine 11 waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi mawili tofauti kwenye mji wa kaskazini wa Beit Lahia na eneo la kaskazini-magharibi mwa mji wa Gaza.
dpa