Mkuu wa ujasusi Venezuela akiri kulangua dawa za kulevya
26 Juni 2025Armando mwenye umri wa miaka 65, anayejulikana kwa jina la utani "El Pollo" (Kuku), alikuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Venezuela, akiwa anahudumu chini ya kiongozi wa zamani wa Venezuela Hugo Chavez.
Carvajal alikiri mashtaka ya kula njama ya kuingiza cocaine nchini Marekani, kushiriki katika ugaidi wa dawa za kulevya kwa maslahi ya kundi la wapiganaji la Fuerzas Armadas Revolucionarias de Colombia (FARC), na makosa yanayohusiana na silaha, hii ikiwa ni kulingana na taarifa ya Wizara ya Sheria.
"Hatua yake ya leo inaonyesha dhamira yetu ya kuwawajibisha maafisa wa kigeni wanaotumia vibaya mamlaka yao kuwaharibu raia wetu," Mwanasheria wa Marekani Jay Clayton alinukuliwa akisema katika taarifa yake.
Carvajal, aliyehudumu kama mkuu wa ujasusi jeshini kati ya 2004 hadi 2011, "huenda akafungwa kifungo cha maisha kwenye gereza la serikali kuu ya shirikisho," kulingana na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya, Robert Murphy.
Marekani na Venezuela hawana ushirikiano wa kidiplomasia tangu 2019
Aidha taarifa zimesema kwamba Carvajal alishiriki katika vurugu, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara na mauaji, ili kurahisisha ulanguzi wa cocaine.
Likinukuu vyanzo vinavyofahamu kesi hiyo, gazeti la Miami Herald lilisema Carvajal alikubali kuzipa mamlaka za Marekani nyaraka na ushahidi unaomhusisha Rais wa sasa wa Venezuela Nicolas Maduro na maafisa wengine wakuu wa Venezuela "katika shughuli mbalimbali zisizo halali, kuanzia ulanguzi wa dawa za kulevya na wizi wa kura hadi operesheni za kijasusi na kuwapatia silaha magenge ya uhalifu".
Caracas na Washington wamekuwa na uhusiano mbaya kwa muda mrefu. Nchi hizo mbili hazina uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 2019. Marekani pia imeiwekea nchi hiyo ya Amerika Kusini vikwazo vya kiuchumi na vikwazo vya mafuta.