Mkuu wa misaada wa UN aitaka Israel kuondoa vizuizi Gaza
14 Mei 2025Fletcher amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba hakuna msaada wowote ulioingia Gaza kwa zaidi ya wiki kumi, na kwamba zaidi ya watu milioni 2.1 wako hatarini kukumbwa na baa la njaa.
Ameitaka jumuiya ya kimataifa kufikiria kuhusu kile watakachowaambia vizazi vijavyo kuhusu hatua walizochukua kukomesha kile alichokiita "ukatili wa karne ya 21 ambao unashuhudiwa kila siku katika ukanda wa Gaza.”
Soma pia: Wataalamu waonya juu ya baa la njaa Gaza
Mratibu huyo wa misaada wa Umoja wa Mataifa amesema, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanafanya kila linalowezekana kujaribu kupeleka misaada Gaza lakini Israel inaendelea kuzuia kuingia kwa misaada hiyo.
Ametoa wito kwa Israel kuacha kuua na kuwajeruhi raia na kuondoa vizuizi vya misaada ya kibinadamu.