Mkuu wa Majeshi ya Israel aidhinisha kuishambulia Gaza
13 Agosti 2025Mkuu wa Majeshi ya Israel, Jenerali Eyal Zamir, ameidhinisha mpango wa mashambulizi makubwa ya kijeshi ya ardhini kwenye Ukanda wa Gaza na kutupilia mbali upinzani wa awali wa mpango huo wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Taarifa ya IDF imesema Zamir ameidhinisha "mpango mkakati mkuu" kwa ajili ya operesheni hiyo ya kijeshi kwenye ardhi hiyo ya Palestina.
Hapo kabla, Zamir aliupinga vikali mpango huo kutokana na kitisho dhidi ya wanajeshi wake pamoja na mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas.
Ingawa bado hakujatolewa ratiba ya mashambulizi hayo, tayari ndege za kivita za Israel zimeshambulia mji mkubwa zaidi huko Gaza kwa siku kadhaa, huku maafisa wa afya wanaoshirikiana na Hamas wakidai kuwa watu 123 wameuawa katika muda wa saa 24 zilizopita.