Mkuu wa jeshi la Uganda atishia kuishambulia Bunia, Kongo
15 Februari 2025Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba amesema katika chapisho lake katika mtandao wa kijamii wa X kwamba wanaweza kuushambulia mji wa Bunia uliopo mashariki mwa Kongo ikiwa vikosi vyote vilivyopo katika eneo hilo havitojisalimisha ndani ya masaa 24.
Kainerugaba, ambaye ana historia ya kuchapisha maoni yenye utata juu ya mambo mbalimbali amesema ana mamlaka aliyopewa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ambaye pia ni baba yake. Lakini hata hivyo msemaji mkuu wa jeshi la Uganda amesema hawawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.
Soma zaidi. Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika wafunguliwa mjini Addis Abbaba
Tishio hilo kutoka kwa afisa mkuu wa kijeshi wa Uganda, ambaye anatazamiwa kuwa mrithi wa baba yake linazidisha hofu kwamba mzozo kati ya vikosi vya Kongo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda unaweza kugeuka na kuwa vita vya kikanda. Siku ya Ijumaa, waasi wa M23 waliingia kwenye mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wa Bukavu.