Mkuu wa Hezbollah aonya mpango wa kupokonywa silaha
15 Agosti 2025Mkuu wa kundi la wanamgambo wa Hezbollah, Naim Qassem, ameonya kuwa mpango wa serikali Lebanon wa kulipokonya silaha kundi hilo unaweza kuibua vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Mapema mwezi huu, serikali ya Lebanon ililipa jeshi la nchi hiyo jukumu la kuandaa mpango ifikapo Agosti 31 na kuidhinisha "malengo" yaliyoorodheshwa katika pendekezo la Marekani kuhusu kuwapoknya silaha Hezbollah.
Qassem ameilaani hatua hiyo na kuitaka serikali ya Lebanon kujiandaa kwa machafuko yanayoweza kutokea katika nchi hiyo ambayo tayari inakabiliwa na mizozo iliyoanza tangu mwaka 1975.
Wafuasi wa kundi hilo wanaona ni muhimu kwao kuwa na silaha za kujilinda dhidi ya Israel huku wale wanaolipinga wakiamini hatua hiyo inadhoofisha uhuru wa nchi na kuiweka nchi katika hatari ya vita.